GEITA: SERIKALI kupitia Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa), imetenga kiasi cha Sh milioni 965.4 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa maji katika kata ya Katoma iliyopo kwenye Jimbo la Geita Vijijini.
Meneja wa Ruwasa Wilaya ya Geita, Mhandisi Sande Batakanwa amesema hayo mbele ya viongozi wa mbio za Mwenge kitaifa mwaka 2024 walipofika kwa kukagua na kuweka jiwe aa msingi katika mradi huo.
Soma pia: Upanuzi chujio la maji mjini Geita asilimia 95
Mhandisi Sande amesema chanzo cha fedha hizo ni mfuko wa maji (NWF) na program ya malipo kwa matokeo (P4R), ambapo chanzo cha maji katika mradi ni Ziwa Victoria na mpaka sasa mradi umegharimu Sh milioni 901.6.
Amesema mradi unatarajiwa kunufaisha wananchi wapatao 11,609 wa Kata ya Katoma yenye vijiji 4, ambavyo ni Itale, Katoma, Nyakazeze na Nyambaya pamoja na Kijiji cha Mnyala kilichopo Kata ya Nkome.
Amesema mradi umehusishaa ujenzi wa tanki moja lenye ujazo wa lita 225,000 kwenye mnara wa mita sita, ununuzi wa bomba na ujenzi wa mtandao wa maji wenye urefu wa Km 27, Ujenzi wa Vituo 21 vya kuchotea maji.
“Mpaka sasa mradi huu umefikia asilimia 85 za utekelezaji wake kwa kukamilisha ujenzi wa miundombinu muhimu,” amesema Mhandisi Sande na kuongeza;
“Kazi inayoendelea kufanyika kwa sasa ni majaribio ya mtandao wa maji kwa kusukuma maji kwenda kwenye tanki pamoja na ujenzi wa vituo vya kuchotea maji,” amesema.
Mbunge wa Jimbo la Geita vijijini, Joseph Kasheku (Msukuma) amesema wakazi wa Katoma na Nkome mbali na kupakana na Ziwa Viktoria, lakini wamekuwa na adha ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa muda mrefu.
Msukuma ameishukuru serikali kwa mradi huo na kuwaomba wananchi kuendelea kuwa na imani na serikali iliyopo madarakani kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa 2024 na uchaguzi mkuu 2025.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa mwaka 2024, Godfrey Mnzava baada ya kukagua ameridhishwa na mradi na kuweka jiwe la msingi huku akiwataka halmashauri na Ruwasa kuzingatia weledi kwenye miradi yao.