Wasira: Nyerere aliandika kitabu kutetea wanawake

DAR ES SALAAM — Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira, amesema Hayati Julius Nyerere aliandika kitabu cha kutetea haki za wanawake akiwa Chuo Kikuu cha Makerere University, lakini hakikuchapishwa hadi alipofariki.

Wasira alitoa kauli hiyo Aprili 10, 2026 katika kongamano la kumbukizi ya Mwalimu Nyerere lililofanyika Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Alisema kitabu hicho, kinachojulikana kama Uhuru wa Wanawake, kililenga kuhimiza usawa wa kijinsia na kupinga mifumo ya kijamii iliyokuwa ikiwanyima wanawake haki katika familia za Kiafrika.

“Mwalimu Nyerere aliweka mkazo mkubwa kwa watu na haki zao. Aliamini wanawake wanapaswa kushiriki kikamilifu katika uongozi na maendeleo ya taifa,” alisema Wasira.

Aliongeza kuwa falsafa ya uongozi ya Nyerere ilijikita katika kulinda uhuru wa taifa, kuimarisha umoja wa kitaifa, kukuza maendeleo ya wananchi na kuendeleza harakati za ukombozi barani Afrika.

Kauli hiyo inaangazia mchango wa kihistoria wa Julius Nyerere katika masuala ya usawa na maendeleo ya kijamii nchini Tanzania.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button