Upanuzi chujio la maji mjini Geita asilimia 95

MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Geita (GEUWASA) imeeleza kuwa mpaka sasa mradi wa upanuzi wa mtambo wa chujio la maji Nyankanga mjini Geita umekamilika kwa asilimia 95.

Mradi wa upanuzi wa chujio la Nyankanga ulikuwa ukitekelezwa na kampuni ya M/S GIPCO Co. Ltd na ulipangwa kukamilika Julai, 2022 lakini haukukamilika kutokana na mkandarasi kusuasua.

Advertisement

Akisoma taarifa kwa niaba ya mkurugenzi mbele ya viongozi wa mbio za mwenge kitaifa 2024 walipotembelea mradi, meneja wa Huduma kwa Mteja wa Geuwasa, Ashraf Remtula amesema kwa sasa mamlaka inatekeleza mradi kwa njia ya Force Akaunti kupitia wataalam wa ndani.

Mradio huo unatarajiwa kukamilika Octoba 30 na unatekelezwa kwa mikataba miwili yenye jumla ya Sh bilioni 1.17.

SOMA: Geita wavunja mkataba na mkandarasi wa maji

Ameeleza, mkataba wa kwanza ni ununuzi wa pampu yenye uwezo wa kusukuma lita laki tatu kwa saa kwa gharama ya sh milioni 199.57 kupitia kampuni ya EQUIPLUS.

Mkataba wa pili ni ujenzi wa mtambo wa kuchuja maji kwa gharama ya sh milioni 971.51 kupitia kampuni ya M/S GIPCO Co. LTD ambapo fedha zote za mradi huo zinatoka Serikali kuu.

“Mpaka sasa sh bilioni 1,03 zimelipwa ambapo shilingi milioni 199.57 ni kwa ajili ya ununuzi wa pampu na kiasi cha shilingi milioni 833.74 ni kwa ajili ya kazi za upanuzi wa mtambo.

“Mradi huu wa upanuzi wa chujio utaweza kuzalisha lita milioni 3 kwa siku na hivyo kuongeza uzalishaji wa majisafi kutoka lita milioni 4 kwa siku zinazozalishwa sasa mpaka lita milioni 7 kwa siku,” ameeleza Ashraf.

Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa mwaka 2024, Godfrey Mnzava ameelekeza shughuli za ukamilishaji wa mradi zifanyike kama ilivyopangwa ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama.