Sababu zatajwa wengi kugombea ubunge

KUKUA kwa demokrasia na watu kutaka kujulikana kwenye vyama na kwenye mamlaka za uteuzi zimetajwa kuwa sababu za kuwa na idadi kubwa ya watu wanaochukua fomu za kuomba ridhaa ya kugombea ubunge kuelekea Uchaguzi Mkuu.
Wasomi na wachambuzi wa siasa wameeleza hayo walipozungumza na gazeti la HabariLEO, na kusema demokrasia imeendelea kukua ndani ya vyama na hata kwenye taifa kwa ujumla jambo linalowapa watu wengi fursa ya kugombea nafasi hizo.
Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa na Mwenyekiti wa Chama cha AdaTadea, Juma Ali Hatibu alisema mwamko huo unaonesha ukuaji wa kidemokrasia nchini na hamasa na kuongezeka kwa uelewa kwa vijana na wanawake ambao miaka iliyopita walikuwa nyuma.
“Kumekuwa na hamasa kubwa sana kwa vijana na wanawake, kwangu mimi naona ni jambo jema na zuri kwa sababu kuna watu wana uwezo mkubwa kuliko waliopo sasa kwa hiyo ni jambo jema wanapojitokeza wasomi, vijana, wanawake kwa sababu kila mtu ana haki ya kuchaguliwa,” alisema Khatib.
Alisema zamani wasomi hawakuwa wanapenda kuchukua fomu kutaka kugombea nafasi mbalimbali, lakini sasa imekuwa tofauti kwa kuwa mitazamo hiyo inaendelea kubadilika.
Alisema ili kupata viongozi watakaofaa vyama vya siasa vinapaswa kufuata demokrasia, maamuzi ya wengi wajumbe watakapoamua kiongozi sahihi basi matakwa yao yaheshimike kusiwe na kiongozi flani anamtaka mtu fulani, wakati hana uwezo, wananchi wachague viongozi wanaowataka”.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Richard Mbunda alisema vijana wengi hasa ambao wametoka vyuoni wanaitumia fursa hiyo kwa ajili ya kusogeza majina yao karibu na vyama vyao na karibu na mamlaka za uteuzi.
“Unakuta mtu hana malengo ya kushinda ila lengo lake ni hilo la kusogeza jina kwa sababu ile wanaichukulia kama uwekezaji kwa sababu serikali inapoundwa upya huwa wanaangalia makada wa chama kwenye nafasi mbalimbali za uteuzi kwa hiyo watu wanasogeza wasifu wao waonekane,” alifafanua Dk Mbunda.
Kuhusu kuwapata wagombea wazuri, Dk Mbunda alisema, “Vyama vidhibiti rushwa isitumike kama ndio kigezo cha kupata wagombea, lakini pia wasilete siasa za kushikana mikono kwamba huyu ni mtoto wa fulani basi anapewa fursa”.
Mhadhiri wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Zacharia Swedi alisema mchakato wa kupata wagombea kwa mwaka huu umekuwa tofauti.
Swali alisema ilizoeleka kwamba makada wa vyama au wenye historia ya uongozi ndio wanaopewa nafasi ya kuchukua fomu na hatimaye kugombea, lakini kwa sasa mwanachama yeyote ana nafasi ya kufanya hivyo ndio sababu kumekuwa na mwitikio.
Alisema wingi wa wanaochukua fomu unaweza kuleta hatari ya kumpitisha mgombea asiye sahihi kwa kutomfahamu kama wasipokuwa makini hivyo ni muhimu kufanya ufuatiliaji wa historia ya mhusika juu ya alichofanya na anachotarajia kufanya atakapokuwa katika nafasi anayoihitaji.


