Samaki, viumbe hai wafa Mto Malagarasi

HALI ya sintofahamu imezuka katika Kijiji cha Kigadye, Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma baada ya kutokea vifo vya samaki na viumbe hai wengine kwenye Mto Malagarasi, wakati wananchi wa kijiji hicho wakiwa hawajui sababu ya vifo hivyo.
Wananchi wa kijiji hicho walioshuhudia hali hiyo wakizungumza wakati Mkuu wa Mkoa Kigoma, Balozi Simon Sirro alipotembelea eneo hilo, walisema kuwa hawajui nini kimetokea lakini wanahisi inaweza kuwa sumu.
Enock Emanuel ambaye ni mwananchi alisema walishangazwa na hali hiyo iliyotokea katikati ya wiki iliyopita, baada ya kuona samaki na viumbe hai wengine wa majini katika Mto Malagarasi wamekufa.
Naye mkazi wa Kijiji cha Kigadye kilichopo mpakani mwa Tanzania na Burundi, Richard Sadoki alisema kuwa walishtushwa kuona viumbe hai hivyo vimekufa lakini wanahisi taka za sumu ambazo zinatoka kwenye vimito vidogo vidogo vinavyoingiza maji yake katika Mto Malagarasi vimesababisha hali hio lakini hakuna mtu ambaye
ameathirika.
Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Kigadye, Wilaya ya Kasulu alipotembelea kushuhudia hali hiyo, Balozi Sirro aliagiza uchunguzi wa haraka ufanyike kubaini sababu ya vifo vya samaki na viumbe hai katika eneo hilo la Mto Malagarasi, katika Kijiji cha Kigadye.
Pamoja na kuagiza uchunguzi wa haraka kufanyika kubaini tatizo hilo, Balozi Sirro pia aliwaelekeza wakazi wa kijiji hicho na maeneo jirani kuepuka kutumia samaki hao kwa kitoweo sambamba na kuepuka matumizi ya maji hayo wakati huu serikali ikiendelea na uchunguzi, ili kubaini sababu ya tukio hilo.
Akitolea maelezo kwa Balozi Sirro kuhusu hali hiyo, Ofisa Usafi na Mazingira, Mkoa wa Kigoma, Nesphory Sungu alisema kwa kushirikiana na wataalamu wa afya, tayari wamechukua sampuli ya maji katika maeneo hayo, ili kufanya uchunguzi na kubaini sababu ya tukio hilo.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Dk Damas Kayera alisema mpaka sasa hakuna madhara yaliyokwishatolewa taarifa, huku akitoa wito kwa wakazi watakaobainika kuwa na changamoto za kiafya
kutokana na kula samaki hao, kutoa taarifa kwa watalaamu wa afya haraka.