Samia abeba mambo manne Tanga

RAIS Samia Suluhu Hassan ameainisha mambo manne aliyoyabaini katika ziara yake mkoani Tanga na kuahidi kuyafanyia kazi, ikiwa ni pamoja na kuendelea kuboresha miundombinu ya barabara, maji, ajira kwa vijana na tatizo la migogoro ya ardhi.

Ameyasema hayo alipozungumza na wananchi wa Tanga katika Uwanja wa Mkwakwani.

Amesema tangu alipowasili alipokewa na kuona mabango mengi yakipongeza juhudi zinazofanywa na serikali na utekelezaji wa miradi uliofanyika kupitia fedha iliyoelekezwa huko.

“Nikizingatia niliyoyaona nimebaini suala la miundombinu ya barabara lililojitokeza maeneo mbalimbali.
Nawahakikishia wana Tanga barabara itajengwa yote vizuri na kwa lami japo bado kuna mahitaji na lipo pendekezo la kupanua barabara ya Segera-Tanga, upembuzi umeanza na itawekwa kwenye ilani,” amesema Rais Samia.

Pia, alibainisha suala la upatikanaji wa maji ndani ya mkoa huo kwa wastani yanapatikana kwa asilimia 78 hadi 80 na kuwa kutokana na miradi miwili mikubwa inayoendelea itakapokamilika maji yatapatikana mjini kwa asilimia 95 na vijijini kwa asilimia 90 na kuendelea.

“Suala la ajira kwa vijana kama ilivyokuwa maeneo mengine ya nchi na kote duniani, limejitokeza na jitihada zinaendelea, wanaoijua Tanga wanafahamu kwamba hata wahamiaji wengi wa Tanga walikuja kwa sababu ya bandari yake tayari tumeanza kufufua bandari hiyo, mizigo imeongezeka kutoka tani 400,000 hadi tani milioni 1.2,” alieleza Rais Samia.

Alisema ongezeko hilo la mizigo katika Bandari ya Tanga limeongeza ajira kwa vijana na mpango wa serikali ni kuifanya bandari hiyo kuwa maalumu kwa mbole na kilimo.

Kingine, alichobainisha ni migogoro ya ardhi ambapo alisema ameiagiza Ofisi ya Msajili wa Hazina na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupitia mikataba ya ubinafsishaji wa ardhi ili kubaini kama wenye mashamba hawavunji mikataba.

Katika hatua nyingine, Rais Samia aliahidi kuirudisha Tanga ya viwanda na itakayokuwa kituo kikubwa cha utalii wa fukwe, historia na utamaduni.

 

Aliahidi kulegeza masharti na kutengeneza mazingira mazuri ya uwekezaji ili kuwavutia wawekezaji kufungua viwanda na kutimiza ndoto hiyo.

Alisema maumbile ya Tanga ni kivutio tosha kuanzia fukwe, milima, miinuko na utajiri wa kihistoria pamoja na hulka ya asili ya ukarimu wa watu wa Tanga ambavyo vinaweza kuifanya kuwa kituo kikubwa cha utalii.

“Tanga inaweza kuwa kituo kikubwa cha utalii wa fukwe na utalii wa historia kwa sababu kuna Mapango ya Amboni, Magofu ya Pangani na misikiti ya kale, watu mashuhuri kama Shaaban Robert na utalii wa kiutamaduni,” alifafanua.

Akizungumzia baadhi ya changamoto zilizowasilishwa na Mbunge wa Tanga Mjini, Ummy Mwalimu, Rais Samia alisema kuhusu maombi ya barabara ambazo wabunge wamekuwa wakiomba zijengwe, ikiwemo ya Tanga-Pangani zitawekwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ambayo inaandikwa mwaka huu.

Kuhusu ujenzi wa masoko ya Makorora, Mlango wa Chuma, Mgandini alisema tayari fedha imepatikana kwa ajili ya ujenzi wa masoko hayo.

“Lingine ni Jiji la Tanga kuwa na Chuo Kikuu, hili nimelichukua nitakwenda kulifanyia kazi lakini kwa awamu ya kwanza kupitia mradi wa HEET, Tanga tumeleta Kampasi ya Chuo Kikuu Mzumbe ambacho kitajengwa Mkinga ili kisaidie kuchangamsha Mji wa Mkinga,” alifafanua.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button