Samia afanya makubwa sekta saba

Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Rais Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa kwenye miradi muhimu kutoka sekta saba zinazomgusa mwananchi moja kwa moja.

Sekta hizo ni pamoja na elimu, afya, maji, kilimo, uvuvi, barabara na nishati na utekelezaji huo unaenda sambamba na utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Aliyasema hayo jana wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Mwanza alipotembelea miradi ya maji, shule na ujenzi wa daraja iliyopo Wilaya ya Magu mkoani humo.

Advertisement

Majaliwa alisema ujenzi wa mradi wa tangi la kuhifadhi maji la Kisesa ni mpango wa muda wa kati wa kuboresha huduma ya maji Mwanza ambao unagharimu Sh bilioni 3.54.

Mradi huo ambao umefikia asilimia 93 unafadhiliwa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Ufaransa ambapo hadi kukamilika kwake na utahudumia wananchi 75,000 wa maeneo ya Kisesa Bujora, Igudija na maeneo ya jirani.

“Tunataka miradi yote iishe kabla ya kampeni (za uchaguzi mwakani) ili kumrahisishia Rais (Samia) atakapopita kuomba kura, asipate shida,” alisema.

Kuhusu elimu, alisema Rais Samia ameendelea kupanua wigo wa kutolipa ada hadi kidato cha sita, kuongeza fungu la mikopo kutoka Sh bilioni 640 hadi Sh bilioni 760 ili vijana wengi wanufaike.

Alisema Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Mwanza kuanzia Januari itakuwa na wanafunzi zaidi ya 600 na hakuna sababu ya wazazi kushindwa kupeleka watoto wao shule.

“Hakuna mradi utakaolala na badala yake tutaisimamia kuhakikisha inakamilika kwa wakati na kuhudumia wananchi. Tumedhamiria kuwafikia wananchi wote kwa kuwapatia huduma wanazohitaji kwa kutoa fedha kwa halmashauri kutekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo,” alieleza.

Katika afya, wamejenga zahanati kwa ajili ya kupanua wigo wa upatikanaji wa matibabu ya awali na imetoa Sh milioni 700 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Magu na tayari imekamilika.

Majaliwa alisema fedha hizo ni kwa ajili ya ujenzi wa jengo la Mama na Mtoto, wodi ya wanaume, maabara na kuimarisha maeneo mengine kuwezesha wananchi kutibiwa bila kwenda Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza.

Aliongeza kuwa Mkoa wa Mwanza umechangia katika kuinua sekta ya kilimo kwa kuongeza upatikanaji wa mazao ya biashara na chakula na kuifanya Tanzania kuwa eneo muhimu linalotegemewa katika uzalishaji wa chakula Afrika.

Pia, alisema katika sekta ya nishati, Rais Samia amefanya kazi kubwa ya kusambaza nishati ya umeme katika vijiji mbalimbali nchini na vijiji 81 kati ya 82 vya Magu vimeunganishwa na nishati hiyo na kwamba mwananchi anayehitaji ataunganishwa kwa gharama ya Sh 27,000.

Akizungumzia ujenzi wa barabara, madaraja na mifereji, aliutaka Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) ili kukamilika kati ya Aprili na Septemba 2025 kwa lengo la kuunganisha maeneo hayo na kurahisisha upatikanaji wa huduma.

“Daraja la Sukuma linalounganishwa na Bariadi, ujenzi umeanza na litazinduliwa na Rais Samia. Pia, tunajenga daraja kubwa linalounganisha Mkoa wa Mara na ujenzi wa mifereji ya mawe,” alisisitiza.

Kuhusu uvuvi, Majaliwa alisema Rais Samia anatoa boti na nyavu kwa ajili ya kuongeza ufanisi katika sekta ya uvuvi.

“Samaki wanahitajika ndani na nje ya nchi, hivyo hatuwezi kumpa mtu mmoja mmoja vitendea kazi hivi bali kwa ushirika mtasaidika na itakuwa fursa ya kujiongezea kipato,” alisema.

Kwa upande wake, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso alisema wizara hiyo itaendelea kusimamia maagizo ya Rais Samia ya kuhakikisha wananchi wanapata maji katika maeneo yao ili kupunguza adha ya maji.

Alisema ifikapo mwaka 2025, Magu Mjini wawe na asilimia 90 ya huduma za maji na vijijini asilimia 85 na kwamba kuna miradi minane ya Sh bilioni 18 na wanaamini ifikapo mwaka huo, watakamilisha kwa asilimia 88.

“Katika shule (ya Wasichana ya Mwanza) hii tumechimba kisima cha lita 1,700 na mahitaji yaliyopo ni lita 16,000 hivyo niwaombe muongezee pampu itakayosukuma maji ili wanafunzi wasipate usumbufu,” alisema.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA), Nelly Msuya alisema matangi mengine yatajengwa katika maeneo ya vilima vinavyozunguka Mji wa Mwanza ikiwemo Nyamazobe (lita milioni 10), Buhongwa (lita milioni 5), Fumagila (lita milioni 10) na Usagara (lita milioni 1).

“Utekelezaji wa mradi huu wa thamani ya Shilingi bilioni 49 umeanza na unatarajiwa kukamilika ndani ya miaka miwili ifikapo Desemba 2026,” alisema.

Aidha, alisema kuwa ujenzi wa tangi la Kisesa lenye ujazo wa lita milioni tano, unatarajiwa kukamilika ifikapo Februari, 2025.