Samia ageukia shule za wavulana za sayansi

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema katika utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa shule za sayansi, serikali imeanza na wasichana na kuwahakikishia wananchi wa Tanga kuwa baada ya mradi huo kwa wasichana kukamilika, serikali itaanza kujenga shule za sayansi kwa wavulana.

“Kwa namna hii tutahakikisha kuwa wanafunzi wote wanaoanza masomo ya sekondari wanamaliza elimu hiyo, ujenzi wa mabweni kuwaondoshea adha ya usafiri kwa wanafunzi kutembea umbali mrefu kufika shuleni na kuwaepusha na changamoto wanazokutana nazo njiani hii hatua njema sana inayowafanya wanafunzi wakamilishe ndoto zao,” amebainisha Rais Samia.

Rais Samia ameyasema hayo wakati akizindua Shule ya Sekondari ya Sayansi ya Wasichana Mkoa wa Tanga
iliyojengwa wilayani Kilindi.

Rais Samia amesema shule hiyo ina mabweni 12 na darasa la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na kueleza kuwa ni vyema wanafunzi wakapata elimu hiyo mapema ili wakitoka hapo wasibabaishwe na ulimwengu.

Kuhusu changamoto ya usafiri kwa wanafunzi wa shule hiyo na ombi la jenereta la kufua umeme, alisema ofisi yake itayashughulikia.

“Kama mama, kama bibi nimekubebeeni mzigo wa kupata gari na jenereta ili msome. Watoto na wajukuu zangu fursa hii hawaipati wote. Nawaomba mtumie vyema fursa hii, someni mambo mengine ya dunia yapo na mkitoka huku yanakuwa mazuri zaidi kuliko yalivyo sasa, kwa sasa someni,” amewafunda wanafunzi wa shule hiyo.

Alipendekeza kwa uongozi wa Mkoa wa Tanga kama watapenda waipe shule hiyo jina la mbunge wa zamani wa Kilindi, Beatrice Shelukindo ili kuienzi dhamira ya mbunge huyo kupigania elimu kwa watoto wa jimbo lake.

Shelukindo alikuwa Mbunge wa Jimbo la Kilindi katika Bunge la Tisa na la 10 kuanzia mwaka 2005 hadi 2015. Pia, alikuwa Mbunge wa Bunge la Kwanza la Afrika Mashariki kuanzia mwaka 2001 hadi 2005 alipojitosa kuwania ubunge Kilindi. Alifariki dunia Julai 2, 2016 mkoani Arusha.

Rais Samia amewapongeza viongozi wa Kilindi kwa kuwezesha kujengwa kwa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Mkoa wa Tanga, na pia aliwashukuru wanakijiji waliokubali kutoa eneo la ujenzi akisema wameonesha namna  wanavyopenda maendeleo.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Deogratius Ndejembi, kwa niaba ya Waziri wa Tamisemi, amesema Rais Samia ametoa Sh bilioni 116 kujenga shule hiyo ya Kilindi kama hiyo katika mikoa yote ya Tanzania Bara.

“Na hivi tunavyozungumza kila mkoa yaani mikoa 26 tayari ina shule kama hii ambayo umeizindua hapa kwa ajili ya watoto wa kike kuweza kupata elimu,” amesema Ndejembi.

Katika hatua nyingine, Rais Samia amesema serikali itaendelea kuuboresha Mkoa wa Tanga katika sekta mbalimbali zikiwamo kilimo, barabara, elimu, biashara na masoko.

Amesema serikali inachukua hatua ili kuchochea na kukuza uzalishaji katika maeneo yote ambao una historia ya kufanya vizuri katika kilimo cha mkonge, chai, mazao ya matunda na viwanda vikiwamo vya saruji, sabuni na matunda.

Rais Samia alisema miongoni mwa hatua hizo ni kuanzishwa mashamba matano ya malisho ya mifugo na kupeleka vifaa vya kupima udongo ili kuimarisha uzalishaji katika kilimo.

“Pia, tulianzisha soko la madini katika Mkoa wa Tanga ambalo limekuwa na manufaa mengi kwa halmashauri na kwa wananchi wa Tanga. Niwahakikishie kuwa serikali itaendelea kuchochea uzalishaji zaidi ili kuongeza mzunguko wa fedha na kuimarisha ustawi wa mtu mmoja mmoja,” amesema Rais Samia.

Alisema pia, serikali inafungua na kuimarisha njia za usafiri ukiwamo Mradi wa Barabara ya Handeni – Kiberashi – Kijungu – Chemba – Kwa Mtoro mpaka Singida yenye urefu wa kilometa 461.

“Ninafurahi kuwajulisha kuwa utekelezaji wa mradi huu umeanza na tutaufanya kwa awamu. Tumeshaanza Awamu ya Kwanza ya Handeni – Makuleta yenye urefu wa kilometa 20 na Makuleta – Kileguru yenye urefu wa kilometa 30,”
alieleza.

Alisema serikali itaendelea kukamilisha maeneo yaliyosalia ili kuuunganisha Mkoa wa Tanga na Singida ili kufungua
fursa za uwekezaji na ajira kwa vijana.

Alisema ana uhakika serikali ikifungua barabara hiyo vijana watajituma na kusogea zaidi katika maeneo ya biashara.

Aidha, Rais Samia alisema serikali imeimarisha huduma za jamii mkoani humo na imekamilisha hospitali tatu za wilaya, vituo vya afya, zahanati tisa na ujenzi wa majengo ya dharura.

Katika hatua nyingine, Rais Samia amemuagiza, Ndejembi aweke kambi Kilindi ashughulikie migogoro ya ardhi, aimalize, akisema kuishi bila migogoro hiyo inawezekana.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button