Samia aipa maagizo Mahakama Dira 2050
RAIS Samia Suluhu Hassan ameagiza Mahakama ya Tanzania itekeleze mambo 12 kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2050.
Rais Samia aliyasema hayo kupitia hotuba yake iliyosomwa na Makamu wa Rais, Balozi Dk Emmanuel Nchimbi wakati wa maadhimisho ya Siku ya Sheria na kuzinduliwa kwa mwaka mpya wa shughuli za kimahakama wa 2026.
Kaulimbiu ya maadhimisho haya ni ‘Mchango wa Mahakama katika Ustawi wa Maendeleo ya Taifa’, ujumbe ambao unaonesha mahakama ni nguzo muhimu ya ustawi wa jamii, maendeleo ya kiuchumi na ustawishaji wa amani katika taifa.
SOMA: Tanzania yapewa heko huduma za Mahakama
Alisema mahakama ina wajibu muhimu wa kulinda utawala wa sheria, kusimamia utekelezaji wa mikataba, kulinda rasilimali za taifa, na kuhakikisha kuwa maendeleo yanayopatikana yanawanufaisha Watanzania wote kwa usawa.
Rais Samia alibainisha maeneo ambayo mahakama ina mchango mkubwa katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2050 ambayo ni kuendelea kulinda haki na misingi ya Katiba na kuhakikisha migogoro ya kiuchumi, kibiashara na kijamii inatatuliwa kwa haraka na kwa haki.
Alisema pia ni kujenga imani ya wananchi na wawekezaji katika mfumo wa kisheria wa nchi na kukuza uwajibikaji na nidhamu katika utumishi wa umma na sekta binafsi.
Pia, kudumisha amani na mshikamano wa kitaifa, ambao ni msingi wa maendeleo endelevu na kuwezesha mazingira bora ya uwekezaji na ukuaji wa uchumi kwa kuhakikisha utawala wa sheria unazingatiwa.
Rais samia alisema mahakama pia inawajibu wa kulinda haki za makundi maalumu, wakiwemo wanawake, watoto na watu wenye mahitaji maalumu na kuzuia migogoro inayoweza kuwa chanzo cha migawanyiko ya kijamii au kisiasa.
Alisema pia kuharakisha utekelezaji wa sera na mipango ya maendeleo kwa kutoa tafsiri ya kisheria iliyo wazi na thabiti na kujenga na kuimarisha utamaduni wa kuheshimu sheria, haki na taasisi za umma.
Pia, kuchangia katika mapambano dhidi ya rushwa na matumizi mabaya ya madaraka kwa kutoa haki bila upendeleo na kuwezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa kwa kuwahakikishia ulinzi wa haki zao za kisheria.
Rais Samia amewataka majaji na mahakimu wasitumie uhuru wa mahakama kama kichaka cha kuficha uzembe, upendeleo au vitendo visivyo vya haki.
Alisema majaji na mahakimu wanapaswa kutekeleza jukumu lao la utoaji haki kwa kuzingatia masharti yaliyoainishwa kwenye Katiba.
“Kamwe uhuru wa mahakama usitumike kama kichaka cha kuficha uzembe, upendeleo au vitendo visivyo vya haki. Uhuru huo ni dhamana ya kutenda haki kwa uadilifu, uwazi na kwa kuzingatia Katiba na sheria za nchi,” alisema Rais Samia.
Aidha, alisema mahakama si tu chombo cha mwisho cha utoaji haki nchini, bali ni mshirika muhimu katika safari ya maendeleo ya taifa.
“Mahakama inaposikiliza na kutoa maamuzi kwa wakati kwenye mashauri ya jinai, inatoa mchango wake kwa kuimarisha amani na utulivu kwa jamii, na hivyo kuwezesha kufanyika kwa shughuli za kiuchumi na kijamii,” alisema Rais Samia.



