Samia alivyolinda mafanikio urithi wa Bandari za Tanzania

OPERESHENI za bandari nchini Tanzania zimepiga hatua kubwa katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, hali inayoifanya Tanzania kuwa lango muhimu la biashara na usafi rishaji kwa nchi jirani zisizo na bahari.

Ndani ya miaka minne ya uongozi wake, kumekuwa na ongezeko kubwa la mizigo inayoshughulikiwa katika bandari kuu za pwani na zile za maziwa zinazosimamiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA).

Hizo ni pamoja na bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara katika Bahari ya Hindi pamoja na bandari zilizo katika maziwa yakiwamo Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika na Ziwa Nyasa.

Kuhusu mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Samia, Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbossa anasema maendeleo hayo yamechangiwa na miradi ya uboreshaji wa bandari inayoendelea kutekelezwa.

Mbossa anatoa maelezo hayo katika ukumbi wa Idara ya Habari (Maelezo) jijini Dodoma Januari 24, 2025 wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu maendeleo yaliyofikiwa na mamlaka hiyo.

Anasema ukuaji wa biashara katika bandari nchini umechangiwa na miradi ya uboreshaji wa miundombinu tangu, Rais Samia alipoingia madarakani Machi 19, 2021 baada ya kifo cha Rais wa Awamu ya Tano, John Magufuli kilichotokea Machi 17, 2021.

TPA ilianzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Namba 17 ya Mwaka 2004 iliyofanyiwa marekebisho kupitia Sheria Namba 7 ya Mwaka 2019. Mamlaka hiyo inawajibika kusimamia, kuendeleza, kuendesha na kuhakikisha usalama wa bandari kuu nchini zikiwemo za Dar es Salaam, Tanga, Mtwara na bandari za maziwa makuu.

Aidha, TPA inashirikiana na sekta binafsi katika uendeshaji wa huduma za bandari kwa mfumo wa upangishaji maeneo maalumu ya bandari kwa wawekezaji. Kwa ujumla, TPA inasimamia bandari 131 nchini kati ya hizo, 32 zipo
katika pwani ya Bahari ya Hindi huku 99 zikiwa katika maziwa ya Victoria, Tanganyika na Nyasa.

Katika juhudi za kuimarisha uhusiano wa biashara na nchi jirani zisizo na bahari, TPA imeanzisha ofisi za uwakilishi katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Zambia, Burundi, Rwanda, Uganda, Malawi na Zimbabwe.

Kwa mujibu wa Mbossa, TPA imepiga hatua kubwa tangu Serikali ya Awamu ya Sita ilipoingia madarakani. Katika kipindi hicho, kiwango cha mizigo iliyoshughulikiwa kimeongezeka kwa wastani wa asilimia 15.2 kwa mwaka, kutoka tani milioni 20.8 katika Mwaka wa Fedha 2021/2022 hadi tani milioni 27.6 Mwaka wa Fedha 2023/2024.

Anasema katika Bandari ya Dar es Salaam, kiwango cha mizigo kimeongezeka kwa wastani wa asilimia 13.4 kwa mwaka, kutoka tani milioni 18.7 mwaka 2021 hadi tani milioni 23.9 mwaka 2024. Mbossa anaeleza ongezeko hilo limetokana na miradi ya maboresho ya bandari, hususani Mradi wa Lango la Bahari ya Hindi wa Dar es Salaam (DMGP), ambao sasa unaiwezesha bandari kupokea meli kubwa zaidi.

Anasema idadi ya makontena yaliyoshughulikiwa na bandari zote nchini imeongezeka kwa wastani wa asilimia 12.9 kwa mwaka, kutoka makontena 823,404 mwaka 2021/2022 hadi makontena 1,050,486 Mwaka wa Fedha 2023/2024.

Katika Bandari ya Dar es Salaam pekee, anasema idadi ya makontena imeongezeka kwa asilimia 10.7
kutoka makontena 816,368 mwaka 2021/2022 hadi makontena 998,872 mwaka 2023/2024.

“Ongezeko hili la makontena katika Bandari ya Dar es Salaam limechangiwa na uwekezaji uliofanywa na wawekezaji binafsi DP World Dar es Salaam na Tanzania East Africa Gateway Terminal Limited (TEAGTL),” anasema Mbossa.

Kuhusu mizigo ya nchi jirani inayopita katika Bandari ya Dar es Salaam, anasema iliongezeka kwa wastani wa asilimia 8.5 kwa mwaka, kutoka tani milioni 7.8 mwaka 2021/2022 hadi tani milioni 9.2 mwaka 2023/2024.

“Ongezeko hili limetokana na kuboreshwa kwa ufanisi wa bandari, jambo ambalo limevutia waagizaji na wauzaji wa bidhaa kutoka nchi jirani,” anaongeza. Aidha, anasema mapato ya TPA yameongezeka kutoka Sh trilioni 1.1 mwaka 2021/2022 hadi trilioni 1.475 mwaka 2023/2024.

Mbossa anasema katika Mwaka wa Fedha 2022/2023, mchango wa sekta ya bandari kwenye Pato la Taifa (GDP) ulikuwa Sh trilioni 10.8, sawa na asilimia 7.3 ya Pato la Taifa lililofikia trilioni 148.3. Anaeleza kuwa kuongezeka kwa mapato hayo kumetokana na ongezeko la ada za gati, kutokana na kuongezeka kwa mizigo inayoshughulikiwa na
bandari.

Anasema mapato mengine yanatokana na ada za meli zinazoingia bandarini, malipo ya upangishaji maeneo kwa kampuni za DP World Dar es Salaam na TEAGTL pamoja na ada za meli kubwa zinazotia nanga bandarini.
Katika kipindi cha miezi sita kati ya Julai na Desemba 2024, Mbossa anasema TPA ilishughulikia tani milioni
15.47 za mizigo na hivyo kuvuka lengo la kushughulikia tani milioni 14.60 katika kipindi hicho.

Anasema idadi ya makontena yaliyoshughulikiwa na bandari za TPA kati ya Julai na Desemba 2024 ilikuwa makontena 565,361, ongezeko la asilimia 4.9 ikilinganishwa na makontena 539,013 katika kipindi kama hicho mwaka 2023.

Licha ya mafanikio hayo, Mbossa anasema mamlaka hiyo inakabiliwa na changamoto kadhaa kama vile uhaba wa gati za kuhudumia meli kubwa, miundombinu chakavu na uhaba wa maeneo ya kuhifadhi mizigo.

Ili kukabiliana na changamoto hizo, anabainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita kupitia TPA inatekeleza miradi mbalimbali ya kuboresha ufanisi wa bandari nchini, ikiwa ni pamoja na ununuzi wa vifaa vya kisasa na uboreshaji wa miundombinu ya bandari.

Aidha, anasema DP World imewekeza kiasi cha Dola milioni 250 za Kimarekani (takribani Sh bilioni 675) katika kipindi cha miaka mitano ya awali ya mkataba wake wa uwekezaji.

“Hadi sasa, DP World imewekeza Shilingi bilioni 214.42 katika nyanja mbalimbali za uendeshaji wa bandari, ikiwa ni pamoja na ununuzi na usimikaji wa mashine za kisasa za kushusha na kupakia makontena kwa gharama ya Shilingi bilioni 115.80,” anafafanua.

Mbossa ana matumaini kuwa uwekezaji katika miundombinu ya bandari na ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji kama barabara na reli utaboresha zaidi ufanisi wa bandari nchini Tanzania na kanda kwa ujumla.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button