Samia ampa mikoba Masaju

RAIS Samia Suluhu Hassan amemuagiza Jaji Mkuu wa Tanzania, George Masaju kusimamia mahakama na kuhakikisha haki inatendeka bila kuonea mtu.
Samia alisema hayo jana kwenye hafla ya kumuwapisha Jaji Masaju iliyofanyika mkoani Dodoma na kuongeza kuwa jukumu namba moja la majaji ni kusimamia na kutenda haki.
Alisema matarajio ya Watanzania ni kuona mahakama inasonga mbele katika majukumu yake na kuendelea kutekeleza maazimio ya Tume ya Haki Jinai.
Aidha, Rais Samia alimweleza Jaji Masaju aendelee kuitumia serikali kwa sababu ndiyo inayowezesha mahakama kuendelea kutekeleza majukumu yake.
Katika hatua nyingine, Rais Samia alimpongeza Jaji Mkuu mstaafu, Ibrahim Juma kwa kumaliza utumishi wake bila kuwa na makandokando na kumtaka Jaji Masaju kuiga mfano wake katika shughuli zake.
“Umefanya kazi kubwa sana ya kuendeleza na kuleta mageuzi ndani ya mahakama pamoja na kushikwa mkono na serikali, lakini uongozi wako ndani ya mahakama ndio umeleta mageuzi yale,” alisema Rais Samia.
Alisema miongoni mwa mageuzi aliyoleta ndani ya mahakama ni ya kimiundombinu, kimifumo na kiutendaji.
Rais Samia alieleza kitu kilichomfurahisha zaidi kuwa ni maendeleo ya kiteknolojia ndani ya mahakama ambapo kila kitu kinachotokea na kuendelea ndani ya mahakama kinaonekana wakati huo huo kwenye chumba maalumu.
“Kama jaji kaahirisha kesi, inaonekana moja kwa moja kuwa hii kesi namba fulani imeahirishwa sasa hivi saa fulani. Kesi hii imeshahukumiwa, hii bado nikasema sawasawa hii ndiyo mahakama yetu,” aliongeza Rais Samia.
Alisema katika matumizi ya chumba maalumu cha teknolojia kwenye kuendesha mashauri, Tanzania inashika nafasi ya pili ikiwa imezidiwa na nchi moja duniani.

Kutokana na mageuzi hayo, Rais Samia alimtaja Jaji Mkuu mstaafu, Ibrahim Juma kuwa ameacha historia na urithi wa kutosha kwa Watanzania.
Aliongeza kuwa kutokana na kazi hiyo kubwa na nzuri iliyofanywa na Jaji Juma, amekuza imani ya Watanzania kwa mahakama.
“Najua kwamba katika miaka mitatu mfululizo, kila tukifanyiwa tathmini duniani imani ya Watanzania kwa mahakama yao imekuwa ikipanda, tunakushukuru sana,” alifafanua Rais Samia.
Alieleza kuwa katika kipindi chake kazini, Jaji Juma amekuza ushirikiano na mihimili mingine ya dola kwa sababu ili dola iende vizuri, mihimili hii lazima ishirikiane,” aliongeza.
Aliwakumbusha wote waliokuwa wakifikiri kuwa mahakama kushirikiana na serikali ni dhambi, kwamba sivyo, ndiyo maana katika kipindi chake mahakama imepata majaji wengi zaidi.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alimpongeza Rais Samia kwa kutekeleza majukumu yake kwa mafanikio na kwamba Watanzania wenaona namna nchi inavyopaa kimaendeleo.

Alisema mafanikio hayo yanaoneshwa katika miradi inayoendelea kama ya Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato na uzinduzi unaotarajiwa kufanywa wa Daraja la Kigongo-Busisi wiki hii.
Majaliwa alimpongeza Jaji Mkuu Masaju kwa kuonekana, kuteuliwa na kuapishwa kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania akisema utendaji wake ndio umempa mafanikio na kumfikisha alipo.
Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson alisema bunge litaendelea kushirikiana na mahakama kikatiba kwa kuwa kila mhimili una majukumu yake yaliyoainishwa na katiba ya nchi.
Alimtaka Jaji Mkuu Masaju kuhakikisha Watanzania wanapata uelewa na kutofautisha kazi za kila mhimili kuanzia bunge ambalo ndilo linatunga sheria huku mahakama ikitafsiri sheria hizo na serikali kuzitekeleza.



