Samia apongeza waliotoa maeneo mradi wa maji Busega

RAIS Samia Suluhu Hassan amewapongeza wananchi wa Wilaya ya Busega kwa kutoa maeneo yao bure kwa serikali kwa ajili ya kujenga mradi wa maji uliopo Nyashimo wilayani humo katika Mkoa wa Simiyu.
Alitoa pongezi hizo jana Akihutubia wananchi wa Wilaya ya Busega baada ya kufungua mradi wa maji wa Lamadi wenye thamani ya Sh bilioni 12.83.
Alisema kitendo cha kuridhia kutoa eneo bure, wananchi wameonesha uzalendo wa hali ya juu kwa taifa. Alisema hatua hiyo pia inaharakisha maendeleo kwani wangedai fidia miradi isingekamilika kwa wakati.
Aliwaomba wananchi wengine, hususani wilaya za Maswa na Meatu kuiga uzalendo huo ili kuharakisha miradi mbalimbali kukamilika na kuleta manufaa kwa jamii.

Kuhusu mradi huo, alisema utakuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi wa Simiyu kwa sababu utasaidia katika uzalishaji wa chakula kupitia kilimo, upatikanaji wa maji pamoja na usafi wa mazingira.
Aliweka wazi kuwa mradi umebeba upatikanaji wa maji ya uhakika, kilimo, ufugaji na uoto wa asili.
Aliwasisitiza wananchi kutunza mazingira ili kuifanya miradi ya namna hiyo idumu. Aliwataka kujikita zaidi katika kupanda miti badala ya kukata miti.
Sambamba na hayo, alibainisha kuwa upatikanaji wa maji safi na salama unapunguza na kuondoa hatari ya magonjwa kwa jamii.
Rais Samia aliiagiza Wizara ya Maji kushirikiana na mikoa na halmashauri zote ili kuharakisha upatikanaji wa maji safi na salama nchini.



