RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amefanya mabadiliko ya Makatibu Tawala wa Mikoa watatu pamoja na kuwahamisha vituo vya kazi makatibu tawala wengine watatu.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu leo Machi 16, 2023 imeeleza kuwa pamoja na mabadiliko hayo pia Rais Samia amefanya uteuzi wa Kamishina wa Mamlaka ya Kudhibiti Dawa za Kulevya.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa Rais Samia amemteua Ally Senga Gugu kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma, kabla ya uteuzi huo Gugu alikuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara.
Tixon Tuyangine Nzunda ameteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nzunda anachukua nafasi ya Willy Machumu ambaye amestaafu.
Rais Samia amemteua Gerald Msabila Kusaya kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa, kabla ya uteuzi huo Kusaya alikuwa Kamishna wa Kudhitibi Dawa za Kulevya.
Taarifa imesema Aretas James Lyimo ameteuliwa kuwa Kamishna wa Kudhitibi Dawa za Kulevya, akichukuwa nafasi ya Gerald Kusaya ambaye ameteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa.
Pia Rais Samia amewahamisha vituo vya kazi makatibu tawala watatu, ambapo Dk Fatuma Ramadhani Mganda amehamishwa kutoka Mkoa wa Dodoma na kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida. Dk Mganga, anachukua nafasi ya Dorothy Aidan Mwaluko ambaye amestaafu.
Rashid Kassim Mchata amehamishwa kutoka Mkoa wa Rukwa kwenda Mkoa wa Pwani. Mchata anachukuwa nafasi ya Zuwena Omary jiri ambaye amehamishiwa Mkoa wa Lindi.
Zuwena Omary Jiri amehamishwa kutoka Mkoa wa Pwani na kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi anachukuwa nafasi ya Ngussa Dismas Samike ambaye kwa mujibu wa taarifa hiyo atapangiwa kazi nyingine.