Samia awakumbuka watoto waishiyo kwenye mazingira magumu

DODOMA: Rais Samia Suluhu Hassan amewafuturisha Watoto wanaolelewa katika Makao ya Taifa ya Watoto Kikombo Dodoma.

Akizungumza wakati wa Iftari hiyo kwa niaba ya Rais yake, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mwanaidi Ali Khamis alisema alimshukuru Rais Samia kwa kuendelea kuweka mazingira wezeshi kwa lengo la kuwaondolea changamoto watoto wanaishi katika mazingira hatarishi.

“Kipekee kabisa, ninamshukuru tena Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kufuturisha watoto wanaoishi katika Makao ya Taifa ya Watoto Kikombo pamoja na maeneo mengine ya nchi hususani Watoto wa Mkoa wa Arusha na Dar Es Salaam.”

Aidha, Mwanaidi aliongeza kuwa Wizara inatambua na kuthamini mchango unaotolewa na wadau kwa lengo la kuhakikisha watoto walio katika mazingira hatarishi wanapatiwa huduma ya malezi ya muda mfupi katika Makao ya Watoto.

“Serikali na Wadau tutaendelea kushirikiana kutoa huduma kulingana na sheria, kanuni na miongozo tuliyojiwekea, nitumie fursa hii kuwaomba wamiliki wa makao ya kulelea watoto kuhakikisha mnatoa huduma kwa mtoto kwa kuzingatia maslahi mapana ya mtoto.”

Mwanaidi alitumia fursa hiyo kuwapongeza viongozi, walezi na watendaji wa Wizara kwa kuendelea kuratibu na kusimamia utekelezaji wa afua za malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto katika makao yote hapa nchini.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk John Jingu amewasihi watoto waishio katika makao hayo kuishi kwa upendo na amani huku wakiweka bidii katika masomo yao na stadi za kazi kwa ujumla ili waweze kufikia malengo yao ya baadae.

Naye Mwakilishi kutoka Shirika la Abbot fund Edna Hauli ameipongeza Serikali kwa juhudi zake katika kuhakiksha watoto wanakuwa salama na kuahidi kuwa shirika hilo litaendelea kushirikiana na Serikali ili kuhakikisha watoto wanapata mahitaji yao muhimu na kuweza kufikia utimilifu wao kama binadamu.

Tukio hilo pia kuliambatana na tukio la kukabidhi vifaa mbalimbali vitakavyosaidia kurahisisha utekelezaji wa majukumu ndani ya Makao hayo.

Vifaa hivyo ni mashine nne za kufulia, printer na mashine moja ya kudurufu, vitabu 1670, jokofu mbili, nguo na mahitaji mengine ambavyo vilitolewa na Shirika la Abbot Fund vikiwa na thamani ya Sh milioni 88.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button