Samia awataka Watanzania wadhamirie kulitumikia taifa

RAIS Samia Suluhu Hassan ameungana na viongozi wengine wa kitaifa nchini kuwatakia heri Watanzania wote katika kuadhimisha miaka 61 ya Uhuru na kuwataka kutumia maadhimisho haya kutafakari na kuweka dhamira ya kulipeleka taifa mbele kwa kasi zaidi.

Pia, Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango pamoja na kutuma salamu za heri katika kuadhimisha Uhuru wa Tanzania amewataka Watanzania kuzingatia suala la kutunza mazingira ikiwemo kuyafanyia usafi maeneo wanayoishi.

Viongozi hao waliyasema hayo kupitia kurasa zao za Twitter walizozitumia kuwasilisha ujumbe kwa Watanzania walioadhimisha jana miaka 61 ya Uhuru wa Tanganyika.

Advertisement

“Imekuwa safari yenye changamoto na mafanikio mengi ambayo taifa letu linajivunia. Tutumie siku hii kutafakari na kuweka dhamira ya kuongeza juhudi na maarifa ya kulipeleka taifa letu mbele na kwa kasi zaidi,” aliandika Rais Samia.

Dk Mpango katika ujumbe wake alisema endapo kila mtu atafagia uwanja wake, dunia nzima itakuwa safi. “Tunao wajibu wa kulinda na kuhifadhi mazingira yetu kwa maendeleo ya sasa na vizazi vya sasa na vijavyo,” aliandika.

Kwa upande wa wachambuzi na wasomi kuhusu miaka 61 ya Uhuru wa Tanzania na maendeleo kiuchumi, walibainisha kuwa hatua kubwa imepigwa katika sekta mbalimbali ikiwemo miundombinu, afya, elimu, kilimo, mawasiliano na madini.

Gabriel Mwang’onda, mchambuzi wa masuala ya siasa na uchumi alisema nchi imepitia mageuzi mbalimbali na kila Rais amepitia changamoto tofauti katika eneo la uchumi.

“Mwalimu Nyerere alifanya vizuri katika kujenga nchi na baadaye alikumbana na changamoto kama vile vita baridi na ubepari,” alisema.

Alielezea kila hatua ambayo marais sita wa Tanzania wamepitia katika kuijenga nchi kiuchumi na sasa maisha yamebadilika sekta nyingi zimekua, akitolea mfano sekta ya afya ambapo sasa kuna hospitali nyingi kubwa zinazotibu magonjwa ambayo hapo awali yalikuwa lazima yatibiwe nje ya nchi.

Mhadhiri Msaidizi wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mbeya, Idara ya Uratibu na Masoko, Samson Mwigamba, kwa upande wake alisema kutokana na umri ambao Tanzania imepata uhuru, yamefanyika makubwa katika kuinua uchumi wa nchi.

Alisema Tanzania ya sasa yenye watu milioni 61.7 kutoka watu milioni 12 wakati wa uhuru, leo imezungukwa na barabara za lami zinazozunguka nchi nzima, reli ya kisasa na kuelekea kwenye kuwa na umeme wa uhakika baada ya Bwawa la Kufua Umeme wa Maji la Julius Nyrere (JNHPP) kukamilika.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *