Samia aweka historia Dira 2050

RAIS Samia Suluhu Hassan ameweka historia ya kuwa Rais wa pili wa Tanzania kuandika Dira ya Taifa ya Maendeleo isiyokuwa na mwelekeo wa itikadi ya kichama.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema dira inayomaliza muda wake ya 2000-2025 iliandikwa wakati wa Serikali ya Awamu ya Tatu iliyoongozwa na Rais Benjamin Mkapa kuanzia mwaka 1995-2005.
Profesa Kitila alisema hayo Dar es Salaam jana alipozungumza na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na waandishi wa habari.
Alisema Dira iliyoandaliwa sasa 2025-2050 ni ya pili kwa nchi isiyo na mwelekeo wa itikadi ya kichama.
Profesa Kitila alisema Rais Samia anatarajiwa kuizindua dira hiyo Julai 17, mwaka huu kwenye ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma na itaanza kutekelezwa Julai Mosi, mwakani.
Alisema tukio hilo ni la kipekee kwa kitaifa na amempongeza Rais Samia kwa kupata fursa ya kuandaa Dira ya Taifa ya Maendeleo itakayoliongoza taifa kwa miaka 25 ijayo.
Profesa Kitila alitaja dira zilizopita zilizoandaliwa kwa msingi wa chama kimoja likiwemo Azimio la Arusha kuanzia mwaka 1967.
“Hii ilikuwa ni dira kamili ya kitaifa ikafuatiwa na Programu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya miaka 15 kuanzia mwaka 1987 mpaka mwaka 2002. Lakini hii ni dira ya pili ambayo haina mwelekeo wa kiitikadi wa kichama,” alisema.
Profesa Kitila alisema dira ya sasa iliwasilishwa bungeni Juni 26, mwaka huu kwa ajili ya kuridhiwa na chombo hicho cha kutunga sheria na akasema serikali imefanya hivyo ili kuipa ulinzi kwamba viongozi wajao wakitaka kufanya mabadiliko yoyote lazima walishirikishe Bunge.
Hatua 12
Profesa Kitila alisema mchakato wa kuiandaa dira ya sasa umepitia hatika hatua 12 ikiwemo ya kuandaa na kuidhinisha miongozo ya kuandika dira iliyokamilika Februari mwaka 2023.
Alisema hatua ya pili ilikuwa Aprili 3, 2023 wakati Makamu wa Rais, Dk Isdori Mpango kwa niaba ya Rais Samia alipozindua mchakato wa kuanza kuiandika dira hiyo.
Profesa Kitila alisema hatua ya tatu ilikuwa ni kuunda vyombo vya kitaasisi vya kusimamia mchakato wa uandishi wa dira uliotekelezwa katika ngazi tatu.
Alitaja ngazi hizo ni sekretarieti ya kuandika dira chini ya Dk Laurence Mafuru, timu kuu ya kitaalamu ya kuandika dira iliyoongozwa na Dk Asha-Rose Migiro na kamati ya uongozi ya dira iliyoongozwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Alisema hatua ya nne ilikuwa ni kufanya tathmini ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2000 hadi 2025 ili kufahamu mafanikio na changamoto zilizojitokeza.
Alitanabaisha kuwa ripoti ya tathmini hiyo ilizinduliwa rasmi Desemba 9, 2023 kwenye mkutano wa kwanza wa kitaifa wa dira na mgeni rasmi alikuwa Rais Samia Suluhu Hassan.
“Hatua ya tano ya mchakato wa dira ilikuwa ni kuchukua maoni ya wananchi na wadau juu ya matarajio yao kuhusu maudhui gani yawepo kwenye dira ya 2050. Nishukuru kuwa zoezi hili lilikuwa pana na la nchi nzima likigusa kila mdau na kila mwananchi,” alieleza Profesa Mkumbo.
Aliongeza kuwa zoezi hilo kwa ujumla wake liliweza kuwafikia watu 1,170,970 na njia saba zilitumika kukusanya maoni ya kuanza utafiti ngazi ya kaya, utafiti kwa njia ya simu, ujumbe kwa njia ya simu, ujumbe kwa tovuti, makongamano, mahojiano na viongozi mbalimbali na semina pamoja na nyaraka mbalimbali zinazoonesha historia ya nchi.
Alisema hatua ya sita ni kujifunza kutoka nchi mbalimbali zilizopiga hatua kubwa ya maendeleo katika mabara mbalimbali ikiwemo Afrika, Asia na Ulaya.
Profesa Mkumbo alisema hatua ya saba baada ya kukusanya taarifa kutoka mataifa mbalimbali, wataalamu walianza uchambuzi, uandishi na uhariri wa taarifa mbalimbali na kutoa rasimu ya nane ya dira.
Alisema hatua ya nane ilikuwa ni kuzindua rasmi Rasimu ya Kwanza ya Dira, Desemba 11, 2023 ambapo Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi aliizindua na kwa mara ya kwanza Watanzania wakapata rasimu ya kwanza.
Alisema hatua nyingine ni kuipeleka rasimu kwa wadau kwa lengo la kupata maoni ya kiuhariri, baada ya hapo ikaundwa rasimu ya pili, kuiwasilisha kwenye baraza la mawaziri likaipitisha Juni 22, mwaka huu na ikawasilishwa bungeni.



