Samia azindua awamu ya pili ugawaji mitungi ya gesi

RAIS Samia Suluhu Hassan amezindua awamu ya pili ya mradi wa kugawa mitungi ya gesi ya kupikia yenye uzito wa kilo sita wenye thamani ya Sh bilioni 8.4.

Mradi wa kwanza wa ugawaji wa mitungi ya kilo sita umekamilika kwa asilimia 97.8 ambao una thamani ya Sh bilioni 4.3 ambako mitungi 99,300 iligawiwa kwa wananchi katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Rais Samia amezindua awamu ya pili kwenye Uwanja wa CCM Jitegemee wilayani Muheza jana akiwa kwenye siku ya tano ya ziara yake ya siku saba mkoani Tanga.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala ya Nishati Vijijini (REA), Advera Mwijage alisema mradi huo wa mitungi 452,445, utagusa maeneo yote nchini na kila wilaya itapata mitungi 3,255 ya gesi ya kupikia.

Mwijage alisema mitungi hiyo itapatikana kwa bei punguzo ya asilimia 50 ili kila Mtanzania amudu gharama za matumizi ya nishati safi, na kwa wakazi wa Tanga watapata mitungi hiyo kwa Sh 17,500.

Alisema kwa kiasi hicho cha fedha, wananchi watapata mfumo mzima wa jiko la gesi unaojumuisha mtungi wenyewe, gesi na kichomeo kwa gharama nafuu.

Alisema REA pia, inaendesha miradi mingine ukiwamo usambazaji wa majiko banifu unaogharimu Sh bilioni 15.2 na majiko zaidi ya 4,200 yamegawiwa kwa wananchi.

Alisema mradi mwingine ni ujenzi wa miundombinu ya gesi asilia katika mikoa ya Lindi na Pwani utakaowanufaisha wananchi zaidi ya 980 wenye thamani ya Sh bilioni 6.82.

“Mradi mwingine ni usambazaji wa mkaa mbadala ambapo serikali inaendelea kununua mashine na kusambaza mkaa mbadala na ununuzi ukikamilika mkaa utasambazwa kote nchini kuwawezesha wananchi wote kunufaika na mradi huu,” alisema Mwijage.

Alitaja mradi mwingine wenye thamani ya Sh bilioni 35.23 ni wa taasisi zinazolisha watu zaidi ya 100 kusambaziwa mkaa mbadala, ambao Jeshi la Magereza linasambaziwa nishati hiyo katika maeneo 211. Hadi sasa tani 55 zimeshasambazwa.

Mwijage alisema Mkoa wa Tanga una miradi minne ya umeme yenye thamani ya Sh bilioni 137. 87, na kwamba nishati hiyo imefikia vijiji vyote 763 kwa asilimia 100.

Alisema kati ya vitongoji 4,531 vya Mkoa wa Tanga, vitongoji 2,382 vimefikiwa na umeme sawa na asilimia 52.6, na kwamba ambavyo havijapata umeme vitakamilishwa katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Akizungumza mbele ya Rais Samia, Meneja Miradi ya Nishati Safi wa Oryx Gas, Peter Ndomba alisema kampuni hiyo imekuwa mstari wa mbele kuwapatia wananchi fursa ya kutumia nishati safi kwa kuongeza upatikanaji wa mitungi ya gesi hasa vijijini.

Alibainisha kuwa juhudi zao zimesaidia kupanua miundombinu ya usambazaji wa mitungi ya Oryx Gas, ambayo sasa inapatikana kwa urahisi katika miji, wilaya na vijijini, lengo likiwa ni kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa.

Alimshukuru, Rais Samia kwa kuipa kipaumbele ajenda hiyo na kueleza kuwa Oryx itaendelea kushirikiana na serikali kuhakikisha wananchi wanapata suluhisho bora la kupikia linalolinda afya na mazingira.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button