Samia: Hakuna mwenye ubavu kuligawa Taifa
RAIS Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa ameamua kunyamaza kimya na ataendelea kunyamaza kimya, lakini hakuna mwenye misuli na ubavu wa kuligawa Taifa wala kuuza Taifa ,au kuharibu amani na usalama wa nchi.
Rais Samia amesema hayo wilayani Arumeru mkoani Arusha kwenye Maadhimisho ya miaka 60 ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) yaliyofanyika Viwanja vya Mfuko wa Wastaafu mkoani Arusha Agosti 21, 2023.
Amesema amesikia yote aliyosema Askofu Dk, Fredrick Shoo kuhusu usalama,amani,umoja wa Taifa. “Nimeyasikia yote ,niliamua kunyamaza kimya na nitaendelea kunyamaza kimya,na hakuna mtu mwenye misuli na ubavu wa kuharibu amani na usalama uliojengwa katika Taifa hili na haya itoshe kuwa ni ujumbe wangu kwenu,” amesema Rais Samia.
Naye Dk Shoo amemuomba Rais Samia kufanya kazi zake kwa kujiamini na ujasiri, kwani Mungu ndiye aliyemuweka na kusisitiza kuwa kanisa hilo linaunga mkono uwekezaji wa suala la bandari.
Amesema kuna watu hawamuamini na hawakutaka kuona mwanamke akiongoza, lakini afanye kazi zake kwa kujiamini na ujasiri, kwani Mungu ndiye amemuweka katika nafasi hiyo na hilo ndilo wanalolisheshimu.