Samia, Majaliwa wahimiza amani

RAIS Samia Suluhu Hassan amewatakia Waislamu heri na mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan akiwataka wananchi waendelee kutunza na kuiombea nchi amani.

Kupitia ukurasa wake katika mtandao wa kijamii wa X Rais Samia ameeleza kuwa katika ibada hiyo wananchi waendelee kuitunza na kuiombea nchi yetu amani.

“Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema atuongoze na kutusimamia kwenye ibada hii muhimu katika imani, aipe kibali cha kheri na kuipokea,” alieleza.

Aliongeza: “Tuendelee kumuomba Mwenyezi Mungu atujalie kila mmoja kwa nafasi yake kuendelea kutekeleza wajibu wake kwa uadilifu, kwa haki na kweli na matokeo ya maisha na kazi zetu yawe yenye kumpendeza yeye, na yenye kulifaa taifa letu na watu wake. Ramadhan Mubarak”.

Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango kupitia ukurasa wake wa X amewatakia Waislamu heri ya mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhan.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kupitia ukurasa wake wa X pia amewatakia Waislamu wote heri ya mfungo mwema akisisitiza kuombea taifa sambamba na kudumisha amani, umoja, upendo na mshikamano miongoni mwa Watanzania.

Ijumaa iliyopita alipomwakilisha Rais Samia wakati maombi ya kitaifa yaliyoandaliwa na umoja wa viongozi wa makanisa Dar es Salaam, Majaliwa alitoa mwito kwa viongozi wa dini waendelee kuliombea taifa na viongozi wake kwa kuwa bila amani na utulivu nchi haiwezi kutimiza malengo ya kuwaletea Watanzania maendeleo ya kiuchumi.

“Nchi haiwezi kuwa na uhuru wa kuabudu, pasipo amani hatuwezi kufanya shughuli za uzalishaji mali. Katika eneo hili ninawapongeza na kuwashukuru madhehebu yote ya dini kwa kuendelea kuiombea nchi yetu amani, mshikamano na utulivu,” alisema.

Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba kupitia ukurasa wake wa X alieleza kuwa huu ni mwezi wa rehema, msamaha na ibada.

“Nawatakia Waislamu wote mfungo mwema wenye baraka na amani,” alisema Dk Mwigulu.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button