Samia: Tunzeni siri za serikali

RAIS Samia Suluhu Hassan ameagiza wafanyakazi wa Chama cha Taaluma ya Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania (TRAMPA) watunze siri za serikali.
Alisema hayo akifungua mkutano wa 10 chama hicho jijini Arusha jana, na kuwashukuru Trampa kwa kutambua kuwa na yeye ni mwanataaluma mwenzao kwa kuwa aliwahi kufanya kazi hiyo katika Ofisi Kuu ya Mipango na Maendeleo Zanzibar.
Rais Samia alisema inasikitisha wakati mwingine kuona kumbukumbu za serikali mitandaoni zikiwamo barua na nyaraka na baadhi ya hukumu zinazotolewa na mahakama jambo linaloweza kuleta uchonganishi ndani ya nchi. Alisema serikali inafanya kazi kwa utaratibu.
“Kafanyeni kazi kwa weledi na kwa uaminifu mkubwa, simameni kwenye maadili na miiko ya taaluma yetu kwa kuzingatia unyeti wa kumbukumbu na nyaraka katika utendaji kazi wa kada hii,”alisisitiza Rais Samia Pia aliwahakikishia watunza kumbukumbu hao kuwa serikali itawalinda kwa hali zote kama walivyoomba kwenye risala kwa kuwa wao ni kitovu cha kazi zote za serikali.
Rais Samia alisema kada ya watunza kumbukumbu na nyaraka ni muhimu kwa kuwa ndio wanaotunza taarifa na kumbukumbu za serikali.
Kwa mujibu wa Rais Samia, watumishi wa kada hiyo ya watunza kumbukumbu na nyaraka na wenzao wa Chama cha Makatibu Mahsusi Tanzania (TAPSEA), wataanza kula kiapo cha uaminifu na kutunza siri katika mkutano wa 11 wa Trampa utakaofanyika mwakani Zanzibar.
Kauli hiyo ya Rais Samia ilikuja baada ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utawala Bora na Utumishi wa Umma wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Haroun Ali Suleiman, kumuomba kuanza utaratibu wa kuwalisha kiapo watumishi wa Trampa kutokana na unyeti wa kazi wanazofanya.
Suleiman pia alimuomba Samia kuwapatia Trampa nishani maalumu kutokana na jitihada za kuimarisha muungano kwa kuwa chama chao kinajumuisha pande mbili za muungano na kiko hai kila upande.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Jenista Mhagama, alisema tatizo la kuwa kwenye daraja moja la mshahara kati ya watumishi wenye stashahada na shahada wa chama hicho tangu kupata uhuru, limeanza kufanyiwa kazi.
Mhagama alisema Rais Samia ameshawaagiza kutenganisha daraja la stashahada na shahada na yeye akamwagiza Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Dk Laurean Ndumbaro, kukamilisha marekebisho ya kanuni ili watumishi hao kila mmoja akae kwenye daraja analostahili.
Mwenyekiti wa Trampa, Josephine Manase alimuomba Rais awasaidie kupata eneo la kujenga ofisi za makao makuu ya chama chao mkoani Dodoma. Samia alilikubali.
Josephine alisema chama kilianzishwa mwaka 2012 kikiwa na wanachama 149 na sasa kina wanachama 4,500 chini ya Mlezi wao, Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi.
Alisema wanazingatia ushauri waliopewa na Mwinyi kwa kuitaka Trampa kuendelea kubaki kuwa chama cha taaluma na si vinginevyo.
Aliyataja baadhi ya mafanikio waliyopata ni pamoja kuungwa mkono na waajiri wengi, kuendesha na kuratibu mafunzo kila mwaka na kufanya kazi na serikali kwa karibu.