Samia: Tusikubali waiharibu Tanzania
RAIS Samia Suluhu Hassan ameonya watu wanaoingilia mambo ya ndani ya Tanzania.
Ameagiza vyombo vya ulinzi na wawakilishi wa Tanzania nje ya nchi wasiwape nafasi watu hao wakiwemo wanaharakati ya kuendelea kuvuruga amani na akasema Tanzania si shamba la bibi.
Rais Samia alitoa msimamo huo Dar es Salaam jana wakati akizindua Sera ya Mambo ya Nje ya Mwaka 2001 Toleo la Mwaka 2024.
“Tusitoe nafasi, walishaharibu kwao, walisha vuruga kwao, nchi iliyobaki haijaharibika watu wako wako usalama amani, na utulivu ni hapa kwetu, kuna majaribio kadhaa, niwaombe vyombo vya usalama na nyinyi mabalozi wetu kutokutoa nafasi kwa watovu wa nidhamu,” alisema.
Aliongeza: “Kama kwao wameshadhibitiwa wasije kutuharibia huku. Niwaombe, katika matamko yanayotoka ni vyema wizara na vyombo vya ulinzi na usalama mkajibu kwa haraka aidha kutoa ufafanuzi, kukanusha au kukubali na kuchukua hatua za kurekebisha lakini tusiwe shamba la bibi kwamba kila mtu anaweza kuja akasema analolitaka, lipo au halipo watu wakajisemea tu.”
Rais Samia alisema kuboresha sera ya mambo ya nje kuna malengo tisa ikiwa ni pamoja na kuimarisha diplomasia ya uchumi kujielekeza kuvutia mitaji mikubwa na kutumia fursa ya kijiografia na kufaidika na soko huru la biashara Afrika.
Alitaja lengo lingine ni kuongeza kasi na uwekezaji katika sekta binafsi mahususi katika ubia kati ya serikali na sekta binafsi ili ni kujenga uhimilivu wa kiuchumi.
Rais Samia alisema pia marekebisho hayo yanalenga kukuza hadhi na kueleza mazuri ya kiuchumi kisiasa na kijamii mila na desturi lugha ya Kiswahili ili kujenga ushawishi na kupanua masoko nje ya Afrika.
Alisema serikali inalenga kukuza ushiriki na ushirikiano na watanzania waishio nje ya nchi na wenye uraia wa Tanzania na wasio na uraia kukuza uchumi na uwekezaji.
Rais Samia alisema kutokana na mabadiliko ya katika uchumi wa dunia serikali imeona ipo haja ya kuja na mbinu ili kupanua mawanda ya kiuchumi ikiwemo kuanzisha maeneo mapya ya uwekezaji na mashirikiano kama sekta ya uchumi wa buluu, uchumi wa kidijiti na sekta ya madini.
Aidha, alisema serikali ina lengo la kuongeza uwazi na uwajibikaji katika diplomasia kupitia diplomasia ya umma na kutumia mifumo ya kidijiti ili nchi itambue kazi zinazofanywa na mabalozi katika nchi wanazoziwakilisha.
Rais Samia alisema mabadiliko ya Sera ya Mambo ya Nje ya 2001 Toleo la 2024 ni matokeo ya mabadiliko na mageuzi ya kiuchumi yaliyotokea nchini katika kipindi cha miaka 24.
Alisema mabadiliko ya muundo wa uchumi yamesababisha kutanuka kwa sekta za msingi kama vile utalii, kilimo, na viwanda na kuibuka kwa uchumi wa buluu, uchumi wa kidijiti na uchumi wa sekta za ubunifu sanaa na michezo.
Mabadiliko hayo yameleta uhusuano wa kimataifa na kuongezeka kwa mahitaji ya masoko nje ya nchi kukuza uchumi.
Alisema uwepo wa majanga ya afya na mabadiliko ya tabianchi, usalama wa nishati, uhalifu wa kimtandao, na ugaidi kunasababisha umuhimu wa sera hiyo kuwa ni hitaji la muhimu.
Rais Samia alisema upo umuhimu wa kubadilisha sera ya mambo ya nje ili kuendana na wakati hasa katika kipindi hiki cha ongezeko la utandawazi na vita ya kibiashara baina ya mataifa makubwa.
Alisema sera hiyo sasa ina misingi minane na ameiagiza Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki itoe mafunzo kwa taasisi za umma, wizara na mashirika, namna sera hiyo inavyogusa maslahi ya taasisi zao.
Aliwataka mabalozi wastaafu watumike kutoa elimu ya sera mpya na kueleza mabadiliko yaliyofanyika.



