Samia: Tutaendeleza majadiliano ya kisiasa

DAR ES SALAAM; RAIS Samia Suluhu Hassan amesema kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025, serikali itaendeleza majadiliano ya kisiasa na kuwajuza wanadiplomasia wote kila kitu kinachoendelea wakati wote wa kipindi cha uchaguzi ili kuwafanya kupata taarifa rasmi na sahihi na sio taarifa za uongo.

Sambamba na hilo, amesema katika kipindi hicho, serikali imejipanga kikamilifu kuendeleza uwazi, uwajibikaji na utawala wa sheria.

Rais Samia alisema hayo jana wakati akizungumza na mabalozi wanaowakilisha nchi zao nchini ambapo alisema maboresho ya sera hiyo yataruhusu jamii ya Watanzania wanaoishi nje ya nchi (Diaspora) kupata hadhi maalumu ili waweze kuwa na mchango katika maendeleo ya taifa lao.

Advertisement

Alisema mwaka 2025 Tanzania itapitia upya Sera ya Mambo ya Nje ili kuboresha Diplomasia ya Uchumi na kufanya uchumi wa nchi kuwa wa kisasa na wa viwanda.

Kadhalika, Rais Samia alisema serikali yake iliendelea kuongozwa na falsafa ya 4R ambapo iliboresha demokrasia na kuanzisha mchakato wa pamoja kisiasa kujenga umoja na mshikamano wa taifa.

“Kupitia juhudi za majadiliano tumetengeneza mazingira yanayovutia majadiliano ya wazi kushajihisha umoja wa kitaifa na kuendeleza demokrasia ya nchi kwa maslahi ya Watanzania wote,” aliongeza Rais Samia.

Alifafanua kuwa majadiliano ya pamoja yamewezesha kuanzishwa mageuzi ya kisiasa na kuwezesha mchakato wa uchaguzi kuwa mzuri zaidi hali iliyowezesha kuwa na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa amani na utulivu mwaka 2024.

Aliongeza kuwa mabadiliko ya sera pia yapitia na kutekeleza utamaduni wa nchi katika msimamo wa diplomasia katika masuala mbalimbali ya kimataifa.

Pia, alisema mwaka huu serikali itakamilisha Dira ya Maendeleo ya Taifa ambapo haitaangalia vipaumbele vya maendeleo ya taifa pekee bali pia itashirikisha wadau wa maendeleo.

Alisema Mwaka 2024 Tanzania iliimarisha ushirikiano na nchi mbalimbali duniani kupitia ziara alizozifanya katika nchi mbalimbali duniani.

“Tulianzisha majukwaa mbalimbali na kufanikisha kusaini mikataba ya ushirikiano katika maeneo muhimu kwa maendeleo ya Tanzania,” alisema Rais Samia.

Aidha, Rais Samia aliwashukuru mabalozi hao kwa ushirikiano kutoka kwa mataifa yao, akisema uhusiano huo sio tu uliongeza biashara na uwekezaji bali pia yamefungua fursa katika sekta za Tehama, uchumi wa buluu, ulinzi na nishati.

“Tutaendeleza ushirikiano ili kukuza uchumi kwa maslahi ya pande zote, kuboresha mazingira rafiki ya kibiashara na uwekezaji,” alisisitiza Rais Samia.

Kuhusu maendeleo ya Tanzania kikanda, alisema mtangamano wa kikanda umeendelea kuwa uti wa mgongo wa Sera ya Mambo ya Nje ya Tanzania ambapo mwaka jana ilipewa heshima ya kuwa mwenyeji wa mkutano wa maadhimisho ya miaka 25 ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Alisema hayo ni mafanikio makubwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa sababu ni maadhimisho yaliyozileta pamoja nchi nane kutoka nchi tatu tangu jumuiya hiyo ilipoanzishwa tena mwaka 1999.

“Mtangamano wa EAC umeongeza kiwango cha biashara kutoka dola za Marekani bilioni 1.8 mwaka 2005 hadi kufika dola bilioni 12.5 mwaka 2023 na kuongeza kiwango cha bidhaa na huduma zinazotolewa ndani ya jumuiya hiyo,” aliongeza Rais Samia.

Alisema kutokana na mtangamano ulioongeza mataifa zaidi, EAC imekuwa na idadi ya watu inayofikia zaidi ya milioni 300 na kuwa na Pato ghafi la jumla ya dola za Marekani bilioni 312.9.

Rais Samia aliwashukuru mabalozi kutokana na mataifa yao kuendelea kuunga mkono ajenda ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya mtangamano.

Aliongeza kuwa Agosti 2024 Tanzania ilipokea uenyekiti wa Asasi ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) inayoshughulikia Siasa, Ulinzi na Usalama ambayo inashughulikia amani na uthabiti wa kikanda.

Aliongeza kuwa kutokana na majukumu hayo, Tanzania ilishiriki katika kusimamia shughuli mbalimbali katika mataifa ya Namibia, Botswana na Msumbiji ambayo yalifanya chaguzi zao mbalimbali mwaka huo.

Kuhusu biashara na uwekezaji, Tanzania ilitengeneza mazingira shindani ya kibiashara na uwekezaji yaliyoiwezesha nchi kuwa kitovu cha biashara na uwekezaji huku uchumi wa nchi ukikua kwa asilimia 5.4 mwaka 2024 ukiongezeka kidogo ikilinganishwa na asilimia 5.3 mwaka 2023.