Samia: Wakishafanya vurugu wanakimbia, msikubali!

HAI: Mgombea urais wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dk Samia Suluhu Hassan amewataka wananchi kutokubali kushawishika na kufanya vurugu zitakazoharibu amani ya Tanzania.
Dk Samia ametoa kauli hiyo leo Oktoba 01, akiwa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro wakati akiendelea na kampeni za kuelekea uchaguzi mkuu badae mwezi huu.
Amesema ni vyema watanzania wakajua gharama za amani taifa inayojivunia na sio wote wanaofurahia Tanzania kuwa kisiwa cha amani
“Msikubali kushawishiwa kuharibu amani ya Tanzania, msikubali hata kidogo, wanaoshawishi wanapo pa kwenda ninataka kuwaambia kukitokea jambo tu tunawarudisha ‘airport’ na ‘passport’ zao mkononi zina VISA tayari wanaondoka familia zao hazipo hapa, wapo wao kufanya fujo kukikorogeka wakimbie wakaungane na familia zao sisi tunakwenda wapi? amehoji Dk Samia na kuongeza kuwa
“Na ndio maana wakishakoroga wakikimbia tunawarudisha kama mmekikoroga kilipuke wote tukiwa hapahapa ndani, sio mlipue halafu muondoke hapana hiyo haikubaliki” amesema Dk Samia.
Mgombea huyo amehitimisha kwa kuwataka wananchi kufika kwa wingi kupiga kura na kurudi nyumbani kusubiri matokeo huku akieleza kuwa vyombo vya ulinzi vimejipanga vyema kuhakikisha usalama unakuwepo.