Sanaa kuitangaza Tanzania nchini India

BALOZI wa Tanzania nchini India, Anisa Mbega ameahidi kuendelea kupanua fursa kwa vikundi vya sanaa na utamaduni kushiriki katika maonyesho mbalimbali nchini India ili kukuza soko la bidhaa na ubunifu wao.
Akizungumza alipotembelea banda la Tanzania kwenye maonesho ya 38 ya Surajkund Crafts Mela huko Haryana, India, Balozi Mbega amesema kuwa ushiriki wa wasanii na wajasiriamali katika matukio kama haya unaongeza mwonekano wa Tanzania kimataifa.
Katika maonyesho hayo, wajasiriamali wa Kitanzania waliuza bidhaa mbalimbali za asili, huku kikundi cha ngoma cha Magoma Moto kutoka Bagamoyo kikiburudisha hadhira na kuonesha utajiri wa utamaduni wa Tanzania.
Maonesho ya Surajkund Crafts Mela, ambayo hujumuisha zaidi ya nchi 50, yalianza Februari 7 na kufikia tamati Februari 23, 2025. Hufanyika kila mwaka na yanaendelea kuwa jukwaa muhimu la kutangaza sanaa, utamaduni, na biashara ya nchi shiriki.



