Sangweni: Mfungamano gesi asilia, kilimo utaongeza tija

DODOMA: ENDAPO sekta za gesi asilia na kilimo zitafungamanishwa vema zitaongeza tija katika uchumi kwani zinategemeana.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Mkundo wa Juu wa Petroli (PURA), Mhandisi Charles Sangweni amesema hayo leo (Agosti 7, 2025) katika banda la mamlaka hilo kwenye maonesho ya Kimataifa ya kilimo (Nanenane)  yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni, Dodoma.

Mhandisi Sangweni alibainisha kuwa, gesi asilia inayozalishwa nchini inaweza kutumika kama malighali kuzalisha ammonia, kemikali ambayo hutumika kuzalisha mbolea za aina mbalimbali ikiwemo urea.

SOMA: PURA yashiriki ukaguzi, majaribio mtambo kuchimba gesi asilia

Alieleza pia kuwa, matumizi ya gesi asilia kwenye magari yamesaidia kupunguza gharama za uendeshaji hivyo gesi asilia ikitumiwa katika magari yanayosafirisha mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi itasaidia kupunguza gharama za usafirishaji.

Kwa upande mwingine, Sangweni alieleza kuwa sekta ya kilimo imeendelea kuwa nguzo muhimu katika utekelezaji wa miradi ya mafuta na gesi asilia kwa kulisha wataalamu wanaofanya kazi katika miradi ya mafuta na gesi asilia nchini.

Pamoja na sekta ya kilimo kutoa huduma hii muhimu, Sangweni alisema bado kumekuwa na changamoto kadhaa ikiwemo kampuni hususan kampuni za nishati za kimataifa kuhitaji bidhaa za kilimo zenye ubora na viwango ambavyo watoa huduma wachache wakitanzania wanakidhi.

Hata hivyo, Sangweni alibainisha kuwa, PURA kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeendelea kufanya jitihada za makusudi kuhakikisha kuwa viwango na ubora hitajika vinafikiwa kwa maslahi mapana ya uchumi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button