Saratani ya Matiti Yazidi Kuwa Tishio

SARATANI ya matiti ni miongoni mwa magonjwa ya saratani yenye athari kubwa kwa wanawake nchini Tanzania. Ingawa siyo ugonjwa unaoenea zaidi kwa wanawake ukilinganisha na saratani ya shingo ya kizazi, saratani ya matiti imeshika nafasi ya pili kwa ongezeko la wagonjwa na vifo vinavyohusiana na ugonjwa huo.
Kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2022 iliyotolewa na Shirika la Kimataifa la Utafiti wa Saratani (IARC) kupitia mradi wa GLOBOCAN, Tanzania iliripoti kuwa kuna wagonjwa 4,502 wanaougua saratani ya matiti, sawa na takribani asilimia 16.9 ya saratani zote kwa wanawake nchini.
Aidha, ripoti hiyo inaonyesha kuwa kiwango cha maambukizi kwa uwiano wa umri (age-standardised incidence rate – ASIR) ni asilimia 19.4 kwa kila wanawake 100,000, hali inayoonyesha ongezeko la maambukizi ikilinganishwa na miaka ya nyuma. Kwa sasa, ugonjwa huu unaendelea kushika kasi ambapo takribani asilimia 80 ya wagonjwa hugunduliwa wakiwa katika hali mbaya (Stage III au IV), jambo linalopunguza uwezekano wa kufanikiwa kwa matibabu.
Uelewa bado ni changamoto
Wataalamu wa afya wanasema uelewa wa jamii kuhusu saratani ya matiti bado ni mdogo. Wanawake wengi hawafanyi uchunguzi wa afya zao mara kwa mara, jambo linalochangia vifo vinavyoweza kuzuilika. Kwa mujibu wa takwimu za kitaifa, ni asilimia 5.2 pekee ya wanawake waliowahi kufanyiwa uchunguzi wa saratani ya matiti, huku wengi wakishindwa kujitokeza kutokana na hofu, gharama au ukosefu wa elimu sahihi kuhusu ugonjwa huo.
Licha ya baadhi ya mitazamo ya kijamii kuona saratani kama ugonjwa “wa kizungu”, wataalamu wa afya wanasema vyanzo vyake vinahusiana zaidi na mtindo wa maisha, mabadiliko ya homoni, umri mkubwa, historia ya kifamilia, unene kupita kiasi na ulaji wa vyakula vyenye mafuta mengi. Utafiti uliofanywa mkoani Kilimanjaro ulibaini kuwa wanawake waliokuwa na mlo wa mafuta mengi walionekana kuwa katika hatari zaidi ya kupata saratani ya matiti.
Huduma na matibabu
Kutambua ukubwa wa tatizo hilo, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa afya imeendelea kuboresha huduma za uchunguzi na matibabu ya saratani nchini. Kwa sasa, tiba ya saratani ya matiti inatolewa katika vituo vikuu vya rufaa kama Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Hospitali ya KCMC, Bugando, na Benjamin Mkapa Hospital, zikitoa huduma za upasuaji, tiba ya mionzi, tiba ya dawa (chemotherapy) na tiba ya homoni.
Hata hivyo, upatikanaji wa huduma hizo bado ni changamoto kutokana na idadi ndogo ya vituo vya rufaa, ukosefu wa vifaa vya uchunguzi kama mammografia na uhaba wa wataalamu bingwa. Wagonjwa wengi huwasiliana na hospitali wakiwa tayari katika hatua za mwisho za ugonjwa, jambo linalopunguza mafanikio ya matibabu.
Kwa sasa, hakuna programu ya kitaifa ya uchunguzi wa mara kwa mara, na wengi hufanyiwa vipimo baada ya kuonyesha dalili za awali. Hata hivyo, kampeni mbalimbali za elimu na uchunguzi zimeendelea kufanyika katika mikoa mbalimbali, zikihamasisha wanawake kujitokeza mapema.
Changamoto na mwelekeo
Changamoto kuu zinazokabili taifa ni pamoja na ucheleweshaji wa kugundua ugonjwa, upungufu wa vifaa vya uchunguzi, gharama kubwa za matibabu, na uelewa mdogo wa jamii kuhusu umuhimu wa uchunguzi wa mapema.Tafiti zinaonyesha kuwa iwapo hatua za kinga na uchunguzi wa mapema hazitachukuliwa kwa haraka, idadi ya wagonjwa wa saratani ya matiti inaweza kuongezeka kwa zaidi ya asilimia 80 kufikia mwaka 2030. SOMA: Saratani yaendelea kuwa tishio
Kutokana na hali hiyo, wadau wa afya wanasisitiza haja ya kuimarisha kampeni za elimu ya afya, kuongeza rasilimali za matibabu na kuweka mpango wa kitaifa wa kudhibiti saratani ya matiti, hususan katika ngazi za jamii. Saratani ya matiti inaweza kuwa tishio kwa afya ya wanawake nchini Tanzania. Hata hivyo, ugonjwa huu unaweza kudhibitiwa ikiwa jamii itahamasika kufanya uchunguzi wa mapema, kubadili mitindo ya maisha na kupata matibabu kwa wakati.
Kwa pamoja, serikali, taasisi za afya na jamii zikiweka nguvu katika elimu, kinga na matibabu, inawezekana kupunguza vifo vinavyosababishwa na ugonjwa huu na kuokoa maisha ya wanawake wengi nchini.