SAU kuchangia 90% akiba ya mwananchi

DAR-ES-SALAAM : CHAMA cha Sauti ya Umma (SAU) kimesema serikali yake itaendeleza sekta ya ufugaji wa nyuki ili kukuza pato la taifa. Ilani ya chama hicho 2025– 2030 imeeleza serikali yake itatoa elimu na kuendeleza teknolojia ya mizinga ya kisasa inayotumia udongo.
“Lengo ikiwa ni kutengeneza mizinga 420,000, yenye uwezo wa kuzalisha kati ya kilo 10 hadi 15 za asali kwa mwaka. “Tunalenga kuzalisha takribani tani 5,066 za asali kwa mwaka, kutoa ajira zaidi ya Watanzania 520,000 pamoja na kuongeza kipato cha wananchi kwa thamani ya kati ya shilingi bilioni 75.9 kwa mwaka kutokana na mauzo ya asali, kwa bei ya jumla ya shilingi 15,000 hadi 30,000 kwa kilo,” imeeleza ilani hiyo.
Chama hicho kimeeleza serikali yake itaunda mfumo wa hifadhi ya jamii utakaowezesha kila Mtanzania, hasa walioajiriwa na wanaojiajiri katika sekta za kilimo na uvuvi kujiwekea akiba. “Serikali itachangia asilimia 90 ya akiba aliyojiwekea mwananchi. Hatua hii inalenga kuwahamasisha wananchi wengi zaidi kushiriki kwenye mifuko ya akiba, kuongeza akiba ya taifa, kukuza uchumi na kuimarisha maisha ya wananchi kwa siku za usoni,” imeeleza ilani hiyo.
SAU imeahidi kuimarisha sekta ya utalii kwa mikakati mbalimbali, ikiwemo kuweka fedha za kufanya tafiti za kihistoria, ili kuyageuza mambo ya kale kuwa vivutio vya utalii vitakavyoongeza ajira na pato la taifa. Ilani imeahidi kuvumbua maeneo mapya ya utalii ikiwemo miji iliyo chini ya bahari na maeneo ya kipekee ya kiasili, kuongeza miundombinu ya malazi kwa kuongeza idadi ya vyumba vya wageni vya viwango mbalimbali pamoja na kukuza utalii wa ndani, ili watanzania wawe miongoni mwa mabalozi wa utalii duniani.
Pia, SAU imeahidi kuendeleza utalii wa fukwe na hifadhi, kwa kusimamia ipasavyo hifadhi za taifa, wanyamapori na baharini kwa kushirikisha jamii za wenyeji. SOMA: SAU: Tutainua wazawa, tutailisha Afrika



