Sauti ya Mitindo yanogesha Miss Universe 2025

DAR ES SALAAM: Katika kuhakikisha mitindo inapewa nguvu na thamani halisi inayostahili, timu ya Sauti ya Mitindo iliyopo chini ya mwanamitindo nguli nchini Miriam Odemba ilikuwepo katika onesho la Miss Universe Tanzania 2025 lililofanyika Super Dome Masaki Dar es Salaam jana.
Sauti ya Mitindo ilifika eneo hilo kujionea namna onesho hilo lilivyopendezeshwa na wanamitindo mbalimbali na baadhi ya wageni kutoka kila kona ya dunia.
Noela Samwel, Caroline Gabriel, Zawadi Joseph, Phillip Dustan na wengine ni wanamtindo wa kutoka Sauti ya Mitindo ambao kwa namna ya pekee walikuwa sehemu ya wanamitindo walioonesha umahiri wao katika onesho hilo.
Katika hatua nyingine, Miriam amesifu walimbwende kutoka Sauti ya Mitindo ambao walihudhuria onesho hilo na timu yake iliyofanikisha uwepo wa eneo hilo.
Miriam Odemba amesema ni shauku yake kubwa timu ya Sauti ya Mitindo kuhudhuriwa kila onesho linalohusu mitindo kwani inatoa thamani halisi ya sekta hiyo kwa lengo la kuikuza na kuipa kipaumbele kwa taifa.
Pia amempongeza Mkurugenzi wa Miss Universe, Millen Happiness Magese kwa kazi nzuri aliyoifanya kuwezesha onesho hilo na kuirudisha kwenye ramani sekta ya urembo.
“Sauti ya Mitindo tupo kwa kushirikiana na hitaji lolote la msaada ushauri au vitu vingine basi tunamkaribisha kwa sababu Sauti ya Mitindo tumebobea katika urembo,” amesema Miriam.
Hakuacha pia kuwapongeza wakongwe wa mitindo walioalikwa kwenye tamasha hilo akiwemo, Asna Hamis, Fiderine Iranga, Martin Kadinda na wengine waliojitokeza.
Sauti ya Mitindo ni jukwaa la mitindo ambalo limeanzishwa na Miriam Odemba kuhakikisha mitindo inafanywa kwa uhakika ubunifu na ustadi.