‘Sekta binafsi, umma zishirikiane kuhusu elimu’

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema kuna haja ya vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki kuimarisha ushirikiano na sekta ya umma na binafsi katika masuala ya elimu ili utoaji wa elimu uweze kuwa wa tija.

Profesa Mkenda amesema sekta binafsi ina nafasi kubwa ya kuchangia uboreshwaji wa elimu kuanzia ngazi ya chini hadi elimu ya juu hivyo kuleta uhalisia wa ushirikiano wa sekta binafsi na umma kwa maendeleo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Akizungumza leo wakati wa ufunguzi wa kongamano la 12 linaloenda sambamba na maonyesho ya ushirikiano kati ya vyuo vya kati, vyuo vikuu na sekta ya umma na binafsi, lililoandaliwa na Baraza la Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki (IUCEA) kwa kushirikiana na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) jijini Dar es Salaam Prof. Mkenda ameeleza umuhimu wa kushirikisha sekta binafsi katika kutafuta suluhu ya kudumu kuhusu changamoto za elimu ya juu ikiwemo uandaaji wa mitaala.

Akitoa mfano wa Tanzania, amesema umuhimu wa sekta binafsi umedhihirika kuanzia ngazi ya chini ya elimu hadi vyuo vikuu.

“Jukwaa hili limechagiza mashirikiano katika kuboresha mitaala kwa kushirikiana na sekta binafsi. Kuimarishwa kwa elimu bora kunahitaji sekta binafsi kuwa mshirika wa karibu,” amesema Prof.

Mkenda na kuongeza kuwa sekta binafsi inamiliki vyuo vikuu vingi zaidi nchini Tanzania ikilinganishwa na sekta ya umma ingawa vyuo vikuu vya umma vinadahili wanafunzi wengi zaidi.

Aidha, Prof. Mkenda ameiomba IUCEA kuja na mpango maalumu utakaokubaliwa na nchi zote ili kufufua mabadilishano ya wanafunzi wa vyuo vikuu na wafanyakazi wa taaluma kati ya nchi hizo ikiwa ni njia ya kuifanya elimu ya juu kuwa ya kimataifa.

“Tufike mahali sasa mwanafunzi wa Kitanzania awe na uhuru wa kuchagua chuo cha kwenda Afrika Mashariki na sifa zake zitambulike. Hii itatusaidia kuendeleza umoja huu wa jumuiya yetu kwa vizazi na vizazi” amesema.

Habari Zifananazo

Back to top button