Sendeka aonya chuki za waliokosa uteuzi

MANYARA : MBUNGE mstaafu wa Jimbo la Simanjiro kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Christoper ole Sendeka amewataka watia nia waliokosa uteuzi wa kugombea katika mchakato wa kura za maoni kuvunja makundi na kuwaunga mkono walioteuliwa na kupeperusha bendera ya chama katika uchaguzi.
Sendeka alisema hayo wakati wa mkutano wa kampeni za mgombea wa urais wa chama hicho, Samia Suluhu Hassan zilizofanyika Babati mkoani Manyara jana. Alisema wanachama wa CCM wanapaswa kuheshimu maamuzi ya vikao vya uteuzi na kuwaunga mkono wagombea walioteuliwa ili kukipa ushindi chama chao. Sendeka alisema wana CCM wanapaswa kufahamu kuwa nguvu ya chama hicho inatokana na umoja miongoni mwao na kukubalika kwa chama hicho na umma.
“Nataka niwaambie viongozi wa mkoa wa Manyara kama kura zako hazikutosha ameteuliwa mwenzako mimi nimeonesha mfano kuumunga mkono James Milya na kuwa mratibu wa kampeni zake katika Jimbo la Simanjiro,” alisema. SOMA: Ole Sendeka aibua jambo bungeni
Aliongeza: “Nataka niwaambie vijana unapoacha kuteuliwa vuta subira”. Wakieleza mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita, mgombea ubunge wa Jimbo la Kiteto, Edward Lekaita alisema wilaya hiyo imenufaika na Sh bilioni 160 za miradi ya maendeleo ikiwemo Sh bilioni 21 katika sekta ya maji.
Naye mgombea ubunge wa Jimbo la Babati Vijijini, Daniel Sillo alisema wamenufaika na Sh bilioni nane katika afya zilizotumika kujenga hospitali ya wilaya, vituo vya afya vitano na zahanati sita. Kwa upande wake, mgombea ubunge wa jimbo la Simanjiro, James Milya alisema jimbo hilo limefanikiwa kujenga shule shikizi 23, pia wamepokea Sh bilioni 44 za miradi ya maji na Sh bilioni tano za ujenzi wa Soko la Madini la Tanzanite ambalo lipo mbioni kukamilika.
Naye mratibu wa kampeni Kanda ya Kaskazini ambaye pia ni Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye alisema mgombea wa chama hicho ni kiongozi mwenye upeo na maono ya mbali. Alisema mgombea wao amezindua Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ili kujenga nchi katika miaka 25 ijayo.