Mkuu wa Mkoa wa Manyara,Queen Sendiga ameshiriki katika kilele cha madhimisho ya siku ya sheria kwa mwaka 2025 Mkoa wa Manyara akiwa mgeni maalumu na mgeni rasmi ni Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Manyara Mheshimiwa John Kahyoza.
Akitoa salamu wakati wa maadhimisho hayo Mkuu wa Mkoa ameeleza kuwa kwa kuzingatia Ibara ya 107A ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, viongozi wa Mkoa wa Manyara wataendelea kuheshimu na kutekeleza maamuzi yanayokuwa yametolewa na Mahakama.
Aidha, Sendiga amewataka wananchi wanaotafuta usaidizi wa kisheria kutumia Mawakili ambao wako rasmi badala ya Vishoka wa kisheria waliopo mtaani.
Naye Jaji Mfawidhi, John Kahyoza amempongeza Mkuu wa Mkoa na wasaidizi wake kwa kuheshimu utawala wa sheria na kutoingilia maamuzi yanayoamuliwa mahakamani.
Aidha, Jaji Kahyoza ametoa rai kwa Viongozi wa dini na mila kuelimisha Jamii kujiepusha na vitendo vya ukatili na ubakaji kwani wahusika wataishia magerezani pale itapothibitika kutenda makosa hayo.
Katika kuhitimisha hotuba yake Jaji Kahyoza amesisitiza kuwa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara itajielekeza kiutendaji ili kwenda sambamba na malengo makuu ya Dira ya Taifa ya maendeleo 2050.