Sera ya Mambo ya Nje iimarishe mtangamano EAC

TANZANIA imezindua Sera ya Mambo ya Nje ya Mwaka 2001 Toleo la 2024 ambapo Watanzania wametakiwa kuitumia kulinda na kutetea maslahi ya taifa na kukuza ushirikiano kimataifa.
Tukio hilo limetajwa kuwa la kihistoria na linalofungua ukurasa wa ushirikiano kati ya Tanzania na mataifa mengine pamoja na jumuiya za kikanda na kimataifa katika nyanja nyingi ikiwemo diplomasia na uhusiano wa
kimataifa.
Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kama taasisi ya kikanda inalengwa kuimarishwa kiuchumi, kijamii na kisiasa na sera hiyo na kuifanya kuwa muhimu si tu kwa Tanzania bali kwa nchi zote za Afrika Mashariki.
Aidha, uzinduzi wa sera hiyo ni kielelezo cha jinsi Tanzania inavyozidi kujiimarisha kisera na nafasi yake kimataifa na utekelezaji wa sera hiyo utazidi kufungua milango ya fursa za kiuchumi, kisiasa na kijamii kwa nchi zote za EAC.
Kwa mtazamo huo, ni dhahiri sera hiyo mbali na mambo mengi ambayo itanufaisha nchi za EAC pia itaboresha mtangamano wa kikanda.
Kubwa zaidi ambalo tunategemea kulipata kutoka katika sera hiyo ni kujengwa kwa mtangamano utakaogusa maeneo yote ya maendeleo kama uchumi, siasa na jamii kwa mataifa yote manane ya EAC.
Lingine ambalo linatia moyo kutoka katika sera ni namna inavyoenda kuhimiza ajenda ya umoja, mshikamano,
amani na utulivu wa taifa, kikanda na kimataifa.
Kwa namna nyingine sera hii imelenga kumaliza matatizo ya kikanda hususani katika nchi za EAC kama migogoro ya wenyewe kwa wenyewe katika mataifa ya ndani ya kanda.
Ni busara kwa mataifa mengine wanachama wa EAC kuhakikisha sera zao zinazingatia maslahi muhimu kwa nchi zingine za jumuiya ili kuwa na kanda yenye utaratibu unaoelewana katika biashara, uwekezaji na maendeleo ya kijamii.
Ikiwa nchi zote za EAC zitakuwa na sera za mambo ya nje zinazopigia chapuo utangamano na ushirikiano wa
kidiplomasia katika maeneo yote ni rahisi siku moja kuwa na sera moja ya mambo ya nje ya EAC.
Jambo la kufurahisha ni kuwa sera hii inalenga kulinda na kutetea rasilimali za taifa na kwa namna moja au nyingine italinda na kutunza rasilimali za kanda katika EAC na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Tunaamini mafanikio ya sera hii katika uchumi wa Tanzania yatakuwa pia mafanikio ya uchumi wa nchi zote zinazounda EAC.



