Serikali: BRT sasa kuendeshwa kwa ubia na sekta binafsi

DODOMA  — Serikali ya Tanzania imetangaza hatua muhimu katika kuboresha usafiri wa umma kwa kusaini mikataba na watoa huduma watatu kwa ajili ya uendeshaji wa Awamu ya Pili ya Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) jijini Dar es Salaam, kupitia ubia kati ya serikali na sekta binafsi (PPP).

Akitoa hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Rais TAMISEMI bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa alisema hatua hiyo ni mwanzo wa zama mpya katika usafiri wa jiji. “Kwa mara ya kwanza, tunasema: subira ya wananchi haikuwa ya bure. Tumefanikisha hatua ya kihistoria,” alisema Mchengerwa mbele ya wabunge.

Mchengerwa hakuweka wazi taarifa zaidi zikiwa ni pamoja na kampuni zitakazoendesha mradi huo, gharama na muda wa mikataba hiyo mipya.

Katika maelezo yake, Waziri Mchengerwa alibainisha kuwa serikali imeanza kusambaza kadi janja 62,000 kati ya 200,000 zinazotarajiwa kwenye awamu ya kwanza, pamoja na kufunga mageti ya kisasa katika vituo vyote 27 vya BRT. Vilevile, mfumo wa kielektroniki wa ukusanyaji nauli (AFCS) umeanza kusimikwa na utaunganishwa na mfumo wa kuongozea magari (ITS), ambao uko kwenye hatua ya manunuzi.

“Hatutaki kurudia makosa ya jana, bali tunajenga mfumo imara, unaozingatia ubora, ufanisi, na heshima kwa maisha ya abiria,” aliongeza Mchengerwa. Alisema usafiri wa mabasi haya hautakuwa tu suluhisho la foleni, bali pia kichocheo cha uchumi na maisha bora kwa wakazi wa jiji hilo.

Waziri huyo alisisitiza kuwa huduma ya BRT ni jibu kwa kilio cha muda mrefu cha wananchi kuhusu usafiri usioeleweka. “Tunajenga mfumo wa usafiri wa heshima, uwajibikaji na thamani kwa kila senti inayowekezwa,” alisema.

Kwa mujibu wa TAMISEMI, mradi huu ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Tawala na dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kuboresha huduma za kijamii kwa kutumia ubunifu na ushirikiano wa sekta binafsi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button