Serikali ilivyofanya mageuzi sekta ya maji

MAJI ni uhai ni kauli ambayo imekuwa ikisemwa na watu wengi kuonesha umuhimu wa maji katika maisha ya Watanzania.
Pia kauli hiyo imekuwa ikisisitizwa mara kwa mara na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan, kuonesha nia yake ya dhati ya kuhakikisha kila mwananchi anafikiwa na huduma za maji safi na salama.
Katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wake, sekta ya maji imepata mageuzi makubwa kupitia ongezeko la bajeti, utekelezaji wa miradi ya kimkakati, na kuimarishwa kwa mifumo ya usimamizi wa rasilimali za maji.
Bajeti iliyopaa
Serikali ya Awamu ya Sita imeongeza bajeti ya maendeleo ya sekta ya maji kutoka Sh bilioni 733 mwaka 2020/2021 hadi Sh trilioni 1.15 mwaka 2024/2025. Uwekezaji huo umechangia utekelezaji wa miradi mikubwa ya usambazaji maji, ikiwemo uchimbaji wa visima virefu, ujenzi wa mabwawa, na ukarabati wa mitandao ya zamani ya maji.
SOMA: Utekelezaji miradi ya maji uendane na mipango ya serikali
Katika hotuba yake bungeni Juni 13, 2024 wakati wa kuwasilisha Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2024/2025, waziri wa fedha Dk Mwigulu Nchemba anasema “Serikali imeongeza bajeti ya sekta ya maji ili kuhakikisha tunafikia malengo ya kitaifa na kimataifa ya maji safi na salama ifikapo mwaka 2030.”
Upatikanaji wa maji vijijini na mijini
Takwimu zinaonyesha kupanda kwa kiwango cha upatikanaji wa maji safi vijijini kutoka asilimia 70.1 mwaka 2020 hadi asilimia 83 Desemba 2024. Kwa upande wa Mijini kiwango hicho kimeongezeka kutoka asilimia 84 hadi asilimia 91.6 katika kipindi hicho.
Wakati wa ziara yake mkoani Ruvuma Januari 28, 2024, Rais Samia anasema: “Nataka ifikapo mwaka 2030 kila kijiji na kila mtaa nchini uwe na huduma ya maji safi na salama. Serikali itaendelea kuongeza uwekezaji katika miradi ya maji vijijini na mijini.”
Miradi mikubwa ya kimkakati
Moja ya miradi iliyokuwa ikisubiriwa kwa muda mrefu ni Mradi wa Same–Mwanga–Korogwe, uliogharimu Sh bilioni 406, mradi huo uliozinduliwa rasmi Machi 8, 2025 na Rais Samia, unahusisha kuvuta maji kutoka Bwawa la Nyumba ya Mungu na una uwezo wa kuzalisha lita milioni 51.6 za maji kwa siku, ukihudumia wakazi zaidi ya 450,000 katika wilaya hizo tatu.
Katika uzinduzi wa mradi huo Waziri wa Maji, Jumaa Aweso anasema mahitaji ya maji katika wilaya za Same na Mwanga ni lita milioni 6 pekee kwa siku, hivyo kukamilika kwa mradi huo kunamaliza kero ya maji katika wilaya hizo na ziada itahudumia maeneo mengine.
Kukwamuliwa kwa miradi chechefu
Serikali ya Awamu ya Sita imekwamua miradi mingi iliyokuwa inasuasua, ikiwemo Same–Mwanga–Korogwe (ulianza 2014, ukakamilika Machi 2025), Bunda (ulianza 2012, ukakamilika 2022), na miradi 177 ya vijijini iliyopachikwa jina la ‘miradi chechefu’.
“Kazi hii imechukua zaidi ya miaka 10, wananchi wakisubiri. Sasa tunakamilisha miradi yote iliyokwama ili wananchi wapate maji bila kuchelewa,” Anasema Rais Samia katika uzinduzi huo uliokuwa umekwama kwa takribani miaka 11. Miradi mingine ni mradi wa ujenzi wa tekeo la maji Kigoma ulioanza kujengwa mwaka 2015 na kukamilika mwaka 2022 takribani miaka 7 baadaye.
Mradi huo una uwezo wa kuhudumia wananchi wapatao 215,000. Upo pia Mradi wa maji Mugango-Kiabakari hadi Butiama ulioanza kujengwa mwaka 2020 na kukamilika mwaka 2025 takribani miaka mitano. Mradi huo unahudumia wananchi zaidi ya 100,000.
Mageuzi ya kitaaluma na kiteknolojia
Sekta ya maji pia imeimarishwa kitaalamu kupitia ujenzi na upanuzi wa maabara za maji. Kufikia mwaka 2024, Tanzania inajivunia kuwa na maabara 17 za kisasa, ambapo saba kati ya hizo zina ithibati ya kimataifa. Hii imesaidia kuongeza ubora wa takwimu na kuimarisha usimamizi wa rasilimali za maji.
Vilevile, kuanzishwa kwa dira za maji za malipo kabla ya matumizi kumeondoa malalamiko ya ankara kubwa zisizoeleweka, kuongeza mapato ya mamlaka za maji na kuboresha ufanisi wa ukusanyaji wa maduhuli.
Gridi ya Taifa ya Maji
Moja ya malengo makuu ya Serikali ya Awamu ya Sita ilikuwa ni kuanzisha Gridi ya Taifa ya Maji itakayounganisha vyanzo vikubwa vya maji kama maziwa, mito na mabwawa.
Akizindua mpango huo jijini Dodoma tarehe 20 Septemba 2023, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa anasema: “Serikali ina dhamira ya dhati kuhakikisha tunaanzisha Gridi ya Taifa ya Maji. Hii itarahisisha usambazaji wa maji kwa miji na vijiji vingi kwa kutumia vyanzo vikubwa vya maji vilivyopo nchini.”
Aina hii ya miradi imeshaanza kutekelezwa ikiwemo mradi wa kutoa maji bwawa la Nyumba ya Mungu kwenda Wilaya za Same, Mwanga na Korogwe; na mradi wa kutoa maji Ziwa Victoria ambao unanufaisha wakazi wa miji ya Kahama, Shinyanga, Tinde, Nzega, Tabora, Igunga na Shelui.
Pia, upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa mradi wa kutoa maji Ziwa Victoria kwenda Dodoma unaendelea huku Wizara ikiendelea na upembuzi huo kwa ajili ya kutoa maji Ziwa Tanganyika kupeleka mikoa ya Katavi na Rukwa kutokea Kigoma.
Mafanikio ya Rais Samia Suluhu Hassan katika sekta ya maji yameweka historia mpya nchini, kupitia uongozi wake thabiti na sera madhubuti, wananchi mijini na vijijini wameona mabadiliko ya kweli kwenye maisha yao ya kila siku katika upatikanaji wa maji.
Maji sasa siyo tena ndoto bali huduma inayoendelea kupatikana, ikiashiria safari ya Tanzania kuelekea uchumi wa kati ulio na ustawi wa kijamii na maendeleo endelevu.



