MKUU wa Mkoa Kigoma, Thobias Andengenye ameutaka Wakala wa Maji Mijini na Vijijini (RUWASA) Mkoa Kigoma kuhakikisha upatikanaji wa vitendea kazi kwenye sekta ya maji unajibu mipango ya Rais Samia katika kusogeza huduma karibu na wananchi (kumtua mama ndoo).
Akizungumza wakati akikabidhi gari kwa ofisi ya Meneja wa Ruwasa Kigoma, mkuu wa mkoa huyo amesema upatikanaji wa vitendea kazi na utekelezaji wa miradi lazima utoe majibu kuhusu kutekelezwa kwa Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inayoitaka wakala huo kuhakikisha upatikanaji wa mkoa mkoani Kigoma unafikia asilimia 85 ifikapo Juni 2025.
Amesema mkoa umefanya kazi nzuri ya utekelezaji wa miradi ya maji tangu Rais Samia alipoingia madarakani ambapo upatikanaji wa maji kwa wananchi umeongezeka kutoa asilimia 58 na kufikia asilimia 74 iliyopo sasa ambapo ametaka miradi 39 iliyopo kwenye mpango itekelezwe kuhakikisha upatikanaji maji kwa wananchi unaongezeka huku akitaka gari hilo kutunzwa liweze kufanya kazi kwa muda mrefu.
Awali Meneja Ruwasa Mkoa Kigoma, Mhandisi Mathias Mwenda amesema kuwa kwa sasa mkoani Kigoma huduma ya maji safi na salama inapatikana kwa asilimia 74 na kutekelezwa kwa miradi 39 ambayo inatarajia kukamilika Desemba 2025 kutaufanya mkoa huo kufikisha asilimia 87 kwa wananchi wake.
Mwenda amesema kuwa upatikanaji wa gari hilo unaondoa changamoto ya ofisi ya meneja wa Ruwasa mkoa Kigoma kuomba gari kwa Meneja wa Ruwasa Uvinza hivyo kuathiri utendaji kazi katika wilaya hiyo.