Shirika lapanda miti utunzaji mazingira

SHINYANGA: SHIRIKA lisilokuwa la kiserikali la Tanganyika Christian Refugee Service (TCRS) limeweka mkakati wa utunzaji wa mazingira kwa kupanda miti na kutoa elimu ya matumizi ya jiko banifu kwa lengo kukabiliana na changamoto ya ukame iliyopo iliyopo wilayani Kishapu mkoani Shinyanga.
Hayo yamesemwa leo na Mwezeshaji wa Utunzaji wa Mazingira kutoka shirika hilo, Emanuel Samweli kwenye Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yaliyofanyika Wilayani humo Kata ya Maganzo.

Samweli amesema kwa kufadhiliwa wa kifedha kutoka Norwegian Church Aid (NCA ) wamekuwa wakitekeleza mradi wa utawala bora,uhifadhi wa chakula na kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi kwa kutunza mazingira kwenye kata za Shagihilu, Bunambiu ,Ndoleleji na Bubiki.
Samweli amesema utunzaji wa mazingira wamekuwa wakiotesha miti na kutumia njia ya matone kwa kumwagilizia na wajasiriamali kuwafundisha namna ya kutumia majiko banifu.
“Tunawafundisha namna ya kutunza visiki hai yaani miti inayojiotea yenyewe na tunawafundisha namna ya kuitunza miti hiyo ya asili na utumiaji wa bajiko banifu ikiwemo umwagiliaji wa kutumia matone”amesema Samweli.

Ofisa Programu kutoka NCA Emanuel Temu amesema wamekuwa wakishughulika na utunzaji wa mazingira kutoa elimu na kuzijengea uwezo kamati za mazingira na klabu za shule za msingi namna ya kukabiliana na majanga na upandaji miti.
Temu amesema wito ni wananchi kuendelea kutunza mazingira kwani dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050 imeeleza kuwajibika na kutunza mazingira na ipo mikoa 15 ya Tanzania bara kwa kutekeleza miradi ya mazingira ikiwemo Shinyanga.
Ofisa Mazingira kutoka Halmashauri ya wilaya Kishapu Kassimu Said amesema wamefanya usafi na zoezi la upandaji miti zaidi ya 300 kijiji cha Masagala huku akisisitiza kuendelea kupanda miti na kuitunza kwani kishapu ni nusu jangwa.

“Makadirio ya upandaji miti ni milioni 1.5 na tunakimbizana na lengo la serikali inagawa utunzaji umekuwa changamoto angalau ifike robo tatu ya miti iliyostawi kwa kupandwa”amesema Said.
Diwani wa kata ya Maganzo Hamza Tandiko amesema wana mradi wa maji yanaopatikana kwa asilimia 85 hivyo watajikita kupanda miti na kuimwagilizia ,mbolea ipo na wanaotelekeza miti watachukuliwa hatua.



