“Serikali inatambua mchango wa sekta binafsi uwekezaji”

SERIKALI inatambua mchango wa sekta binafsi katika uwekezaji na imeendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara kupitia utekelezaji wa Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara Nchini.

Kamishna Msaidizi Idara ya Sera anayeshughulikia masuala ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Masuala ya Kodi na Mwenyekiti wa Kongamano la Kodi, Juma Mkabakuli amesema hayo wakati wa Kongamano la Kodi lililofanyika Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Mkoa wa Mbeya.

Advertisement

Mkabakuli amesema, ili sekta binafsi iweze kushiriki kikamilifu katika kukuza uchumi wa nchi, Serikali inaendelea kuboresha Mazingira ya biashara nchini na imefuta na kupunguza baadhi ya ada na tozo kero takriban 379.

Amesema, Serikali inaendelea kuhakikisha uhimilivu wa viashiria vya uchumi jumla; kuwa na sera za kodi zinazotabirika na kuwianisha tozo na ada mbalimbali zinazotozwa na Wizara na Mamlaka za Udhibiti kwa lengo la kupunguza na kurahisisha ulipaji wake kupitia namba ya malipo jumuishi.

SOMA: Wadau wakutana kujadili mifumo ya kodi

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo- TCCIA Mkoa wa Mbeya, Erick Sichinga, amesema wanaishukuru Serikali kupitia Wizara ya Fedha kwa kuona umuhimu wa kuwa na majukwaa hayo kila mwaka kujadili sera za kodi.

“Mbeya tumebahatika kuwa moja kati ya mikoa ambayo Makongamano haya yanafanyika, nikilinganisha na Kongamano ambalo lilifanyika mwaka jana na mwaka huu nimeona kuwa kuna maendeleo makubwa ambayo sisi wadau wa sekta binafsi, tumeona Serikali imeanza kuwa sikivu, kero mbalimbali zimeanza kufanyiwa kazi, tumeona baadhi ya Maafisa wakipita katika sekta binafsi kwa ajili ya kuchukua maoni na kuyafanyia kazi.” amesema Sichinga.

Sichinga amesema kuwa TCCIA inaendelea kufanya kazi kwa karibu na Mamlaka ya Mapato Tanzania -TRA na hivi karibuni wanatarajia kutia saini makubaliano ya utoaji Elimu kwa Mlipa Kodi kwani Wanyabiashara wengi ni wadau wa TCCIA, lengo kuu ni kuboresha ulipaji kodi kwa hiari.

“Tunataka kuona TRA ni mlezi mkubwa wa biashara yako kwa hiyo kupitia session mbalimbali ambazo TCCIA tunazifanya wadau wetu wanapata elimu”, amesema Sichinga.

Aidha, Sichinga amebainisha majukumu mbalimbali yanayofanywa na TCCIA ikiwemo kuratibu maonesho ya biashara kwa kuwakusanya wafanyabiashara na wazalishaji mbalimbali kwa ajili ya kuonesha bidhaa zao, kuandaa safari za kimisioni za wafanyabiashara (Trade Mission), kutatua migogoro ya kibiashara, kuwawezesha wafanyabiashara wanawake katika sekta ya ujasiriamali, kuibua wafanyabiashara wapya hasa vijana walioko Vyuoni na waliomaliza vyuo pamoja na kuandaa Mabaraza ya Biashara kuanzia ngazi ya Wilaya, Mkoa na Taifa.

Kongamano hilo la Kodi Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Mkoa wa Mbeya limeshirikisha wadau mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara, wajasiriamali wadogo, sekta ya kilimo, biashara za usindikaji wa mazao na washauri wa kodi, ambapo walitoa maoni mbalimbali na kuupongeza Uongozi wa TRA Mkoa wa Mbeya kwa kuwa karibu na wafanyabiashara.