SERIKALI kupitia Wizara ya Fedha imefanya kongamano la kodi kikanda kwa kuwakutanisha wadau kutoka sekta binafsi wakijumuisha wataalam na washauri wa kodi, wadau wa sekta mbalimbali nchini, wafanyabiashara, wazalishaji wa bidhaa na mazao mbalimbali pamoja na makundi maalum ili kuboresha mifumo ya kodi itakayochochea mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji nchini.
Kamishna Msaidizi Idara ya Sera, William Mhoja amesema hayo katika kongamano la kwanza la kodi kikanda kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026, lililofanyika jijini Dodoma.
Mhoja amesema kongamano hilo litasaidia kuboresha uratibu wa ukusanyaji maoni na kuongeza ushirikishwaji wa makundi mbalimbali katika uaandaji wa bajeti ya Serikali na utunzi wa sheria.
“Hatua hii ni moja ya utamaduni wa kutambua mchango wa wananchi kupitia kodi, ada na tozo mbalimbali ambazo zinawezesha ujenzi wa Taifa letu,” amesema Mhoja.
Amesema kuwa lengo la kongamano hilo lilikuwa kupata maoni mbalimbali kwa nchi nzima ikiwa ni pamoja na kupita kwenye kanda ikiwemo Kanda ya Dodoma ambayo ukusanyaji maoni umeanza, Arusha, Mwanza, Kigoma, Mbeya, Iringa na baadae Mtwara na kuhitimisha Dar es Salaam.
Amesema kuwa katika kongamano hilo maoni yote yatakayotolewa na wadau mbalimbali yatafanyiwa kazi ikiwa ni pamoja na kuyafanyia utafiti kabla ya kufanyiwa utekelezaji.
“Hivyo Serikali inawaahidi kwamba maoni yao yanazingatiwa sana kama ambavyo mmeona katika Hotuba za bajeti na Serikali inawakaribisha sana kushiriki na kutoa maoni. Kimsingi maoni ya wananchi wote yanazingatiwa na nawaomba sana wananchi wote wajitokeze kutoa maoni na maoni yao yatafanyiwa kazi kwa sababu mengine yanahitaji kufanyiwa utafiti kwanza kabla ya kuyaleta kwenye utekelezaji,” amesema Mhoja.
Aidha, amewashukuru Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA) pamoja na TradeMark Afrika kwa kushirikiana na Serikali hususan katika kudhamini baadhi ya shughuli mbalimbali katika makongamano haya.
“Ni wazi kuwa ushirikiano huu unalenga kuendelea kukuza uchumi, kuzalisha ajira zaidi na kuwa na maendeleo endelevu” amesisitiza Mhoja.
Kwa upande wa Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania, Alexander Mallya, amewaasa wafanyabiashara kote nchini kutoe maoni yao kuhusiana na masuala mazima ya mapendekezo ya mabadiliko ya kodi.
“Kwa niaba ya Jumuiya ya Wafanyabiashara tunawahamasisha wafanyabiashara wa mikoa yote Tanzania kushiriki makongamano haya yatakapowafikia kwenye kanda zao, kwenye mikoa yao kushiriki kikamilifu na kutoa maoni yao kuhusu suala zima la mapendekezo ya mabadiliko ya kodi,” amesema Malya.
Kongamano hilo ni mwendelezo wa kongamano la kodi kikanda lililoanzishwa na Wizara ya Fedha mwezi Novemba mwaka 2023 ambapo vikao vilifanyika kikanda katika mikoa ya Mwanza, Mbeya, Arusha, Shinyanga, Kigoma, Lindi na Mtwara.