‘Serikali ipo tayari kulipa fidia Sikonge’

SIKONGE, Tabora: NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk, Doto Biteko amesema serikali ipo tayari kulipa fidia kwa wakazi wilayani Sikonge waliopisha ujenzi wa Kituo cha kupokea, kupoza na kusambaza umeme cha Ipole baada ya taratibu zote zinazohitajika kukamilika.

Biteko ameyasema hayo leo Julai 07, 2024 wakati akijibu hoja ya Mbunge wa Sikonge, Joseph Kakunda aliyeiomba serikali kumalizia fidia ya Sh bilioni 2.2 kwa ajili ya wananchi wa eneo hilo wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa Kituo cha kupokea, kupoza na kusambaza umeme cha Ipole, wilayani Sikonge, Mkoa wa Tabora chenye KV 132.

SOMA: Wananchi Ngara kulipwa fidia Sh bilioni 26

Katika hatua nyingine, Mkuu huyo ameagiza kujengwa kwa vituo vidogo vya kupokea, kupoza na kusambaza umeme katika maeneo ya pembezoni ili kukabiliana na tatizo la umeme mdogo (Low votage) na wakati mwingine kukatika mara kwa mara ilhali jitihada kubwa zimefanyika kumaliza tatizo la mgao nchini.

“Kila anayeelewa hawezi kubisha kuhusu kazi kubwa iliyofanywa na Rais, Mhe. Dk. Samia Suluhu Hassan katika uboreshaji wa huduma za jamii, hapendi na anachukizwa na mgao unaochelewesha huduma kwa wananchi,” amesema.

Amesisitiza kujengwa kwa vituo vidogo vya kupokea, kupoza na kusambaza umeme katika maeneo mbalimbali kutadhibiti tatizo la nguvu ndogo ya umeme pale inapotokea hitilafu katika njia kuu ya umeme na pengine utadhaniwa kuwa ni umeme wa nishati ya jua ilhali ni umeme unotoka katika gridi ya Taifa.

Aidha, Dk. Biteko amewataka watendaji wa Shirika la Umeme nchini (TANESCO) na kampuni zake tanzu kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na kwa wakati na kuelekeza apewe ripoti kuhusu hatua iliyofikiwa katika ujenzi wa vituo hivyo ifikapo tarehe 15 Julai, 2024.

“Mwezi machi mwaka huu ujenzi ulikuwa chini sana lakini baada ya shinikizo na usimamizi ujenzi umepanda kwa kiwango kikubwa na hivyo kutatuwezesha kutatua changamoto zinazowakabili wananchi kwahiyo wapeni kazi wakandarasi na kuwasimamia tutapata matokeo,” amesema Dk. Biteko.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mha. Gisima Nyamo – Hanga amesema ujenzi wa kituo cha Ipole utakamilika mwishoni mwa mwezi Agosti mwaka huu na kitou kitawahudumia wananchi wa Skonge, Kitunda na maeneo mengine ya Jirani.

Amesema hadi sasa kituo kimekamilika kwa silimia 97 na kitakuwa kikisambaza umeme kupitia msongo wa KV 33.

Kwa upande wake, Mbunge wa Sikonge, Joseph Kakunda ameishukuru Serikali kwa hatua iliyochukuliwa kufikisha maendeleo kwa wananchi wa eneo hilo na kumtaja Rais, Dk. Samia kama kinara wa maendeleo nchini.

Amesema huduma za umeme imefikishwa katika vijiji 71 vya jimbo hilo na vitongoji 82 kati 187 tayari vimepata umeme huku vingine 15 vikiwa katika mpango wa kuunganishwa katika huduma hiyo.

Habari Zifananazo

Back to top button