KAGERA; KAYA 1339 katika Wilaya ya Ngara wanatarajia kulipwa kiasi cha zaidi ya Sh bilioni 26 ikiwa ni sehemu ya fidia ya ardhi iliyotolewa kupisha mradi wa uchimbaji wa Madini Mkakati ya Nikeli katika eneo la Bugarama mkoani Kagera.
Madini hayo ya Nikeli yatakayochimbwa, yatachenjuliwa na kusafishwa hapa hapa nchini Tanzania kupitia kiwanda cha kisasa kitakachojengwa Kahama mkoani Shinyanga.
Hayo yameelezwa leo Novemba 14, 2023 na Waziri wa Madini Anthony Mavunde wakati wa hafla ya uzinduzi wa ulipaji fidia kwa wananchi waliopisha eneo la Mradi wa Uchimbaji wa Madini Mkakati ya Nikeli iliyofanyika katika viwanja vya mgodi wa Kabanga Nikeli mkoani Kagera.
Mavunde ameeleza kuwa mradi hup ni wa historia katika nchi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara ambao utatumia teknolojia ya kisasa katika uchimbaji na uchenjuaji wa madini hayo nchini ambapo teknolojia itakayotumika ni ya kisasa ya hydro met.
Akielezea kuhusu mipango ya Serikali katika uchimbaji wa Madini Mkakati , Mavunde amebainisha kuwa kwa sasa Serikali inaandaa mkakati wa usimamizi wa madini ya kimkakati na hasa katika kusimamia uongezewaji thamani wa madini hayo hapa hapa nchini.
Aidha, amesisitiza kuwa Serikali inachukua mradi wa Tembo Nikeli kama sehemu ya mradi wa kielelezo kwa miradi mingine ya Madini Mkakati inayofuata.
Kwa upande wa Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi Jerry Silaa amesema kwamba serikali inatambua umuhimu wa mradi huo mkubwa wa kielezo na kwamba wizara ya ardhi itatoa ushirikiano wa kutosha kuhakikisha kwamba zoezi la fidia linakamilika kwa wakati na wananchi wanapata haki yao kwa mujibu wa Sheria.
Wakitoa maelekezo ya Kamati za Bunge za Ardhi,Maliasili na Utalii na Nishati na Madini,Timothy Mnzava na Kirumbe Ng’enda wameitaka Kampuni ya Tembo Nikeli kuhakikisha inalipa fidia kwa wakati kwa wananchi wanaopisha mradi huo wa kimkakati.