Serikali: Iuzieni dhahabu BoT

GEITA: NAIBU Waziri wa Madini, Dk Stephen Kiruswa ameitaka kampuni ya mgodi wa Bucreef Gold Company (BGC) kuangalia uwezekano wa kuanza kuiuzia Benki Kuu ya Tanzania (BoT) dhahabu yote wanayoizalisha.

Dk Kiruswa ametoa maelekezo hayo alipotembelea mgodi huo uliopo Kata ya Lwamugasa wilayani Geita, ambapo serikali kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) inamiliki hisa kwa asilimia 45.

Amesema biashara hiyo inawezekana kwani mwezi Septemba mwaka huu, BoT ilitangaza kuanza kununua dhahabu kwa wachimbaji na wafanyabiashara wa ndani kama sehemu ya kuhifadhi fedha za kigeni.

“Rais Samia (Suluhu Hassan) mama yetu ameamua kwamba tusitegemee dola za wazungu ndio tuweke akiba ya fedha za kigeni nchini, tutumie fedha aliyotupa Mungu ambayo ipo katika madini ya dhahabu.

“Taifa letu lipo katika mchakato kuhakikisha Benki Kuu ya Taifa inaweka akiba ya dhahabu siyo chini ya tani sita kila mwaka, na hiyo dhahabu itatoka kwa achimbaji wadogo wa kati na wachimbaji wakubwa,” amesema.

Kiruswa ameelekeza Bucreef kufanya mapitio ya mikataba waliyoingia na wanunuzi wa nje na kuangalia kama haiwafungi basi waunge mkono hatua hiyo ya serikali ,ili kuiwezesha BoT kufikia malengo yake.

“Kama hiyo mikataba ina ukomo ambao umekaribia, tuiangalie ili dhahabu yote ya hapa isije ikawa inaenda nje na sisi tunatafuta dahabu ya kuisafisha iweze kubaki kwenye akiba yetu ya dhahabu nchini,” amesema.

Meneja Mkuu wa Mgodi wa Bucreef, Gaston Mjwahuzi amekiri kupokea na kuyafanyia kazi maelekezo na kueleza uamuzi wa kuuza dhahabu nje ulikuja baada ya masoko ya ndani kutostahamili biashara yao.

Amesema awali mwaka 2020 Bucreef ilianza kwa kuzalisha takribani kilogram tatu za dhahabu walikuwa wanaiuza soko la dhahabu Geita lakini uzalishaji ulipanda hadi kilogramu 30, uhitaji wa soko la nje ukaja.

Habari Zifananazo

3 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button