Serikali kuendelea kuimarisha uhuru wa kuabudu

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk, Hussein Ali Mwinyi amesema serikali itaendelea kuimarisha uhuru wa kuabudu na kuziagiza taasisi za kidini kuendelea kuiombea nchi amani na umoja.

Rais Dk Mwinyi amesema taasisi za kidini zina wajibu mkubwa wa kushirikiana na serikali na kuunga mkono juhudi za kuleta amani,umoja na mshikamano wa watanzania.

Advertisement

Rais Dk, Mwinyi ameyasema hayo leo alipozungumza katika maombi maalum ya kumpongeza Askofu Agustino Shao kwa utume wake katika Kanisa Katoliki Jimbo la Zanzibar na maombi kwa taifa iliyofanyika viwanja vya Mao Tse Tung Mkoa wa Mjini Magharibi.

Dk Mwinyi amesisitiza kuwa serikali inathamini mchango mkubwa unaotolewa na Kanisa katoliki Jimbo la Zanzibar kwani umekuwa msaada muhimu wa kuimarisha ustawi wa jamii katika nyanja mbalimbali.

Akizungumzia ukarabati wa Kanisa la Minara miwili unaotarajiwa kutekelezwa na kanisa hilo kuwa ni kuunga mkono juhudi za serikali na Shirika la Elimu Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa UNESCO la kuimarisha Mji Mkongwe wa Zanzibar ambao ni Urithi wa Dunia.

Rais Dk.Mwinyi amechangia Sh milioni 100 na Rais Samia Suluhu Hassan amechangia Sh milioni 50 kwa ajili ya ukarabati wa Kanisa la Mtakatifu Joseph liliopo Shangani Wilaya ya Mjini.