Serikali kuimarisha umeme kwenye vitongoji

NAIBU Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amesema serikali inatarajia kuanzisha mradi mpya wa upelekaji umeme katika vitongoji utakaohusisha ujenzi wa njia za kati na ndogo za kusafirisha umeme.

Kapinga ameyasema hayo leo Oktoba 31, 2024 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Mbozi, George Mwanisongole aliyetaka kufahamu ni lini serikali itaanza kupeleka umeme mkubwa kwenye vitongoji ambavyo havijapata umeme mkubwa.

“Kwenye mradi huu utakaoanza Desemba 2024 tumeboresha zaidi kwani tutakuwa na transfoma zenye ukubwa wa KVA 50, 100 na 200 kulingana na ukubwa wa Kitongoji,”amesema Kapinga.

Advertisement

SOMA: Vijiji 76 Newala Vijijini vyafikiwa na umeme

Ameongeza kuwa maeneo ya vitongoji ambayo hayakunufaika na mradi wa awali wa vitongoji 15 yatanufaika kwa mradi utakaoanza Desemba 2024.

Akijibu swali la Mbunge wa Iringa Mjini, Jesca Msambatavangu aliyeuliza ni lini serikali itatekeleza ahadi ya umeme jazilishi maeneo ya miji yenye sura za vijiji kama Ugele, Mosi, Cargrielo, Machinjio, Ulonge, Mtalagala na Msisina, Kapinga amesema serikali inaendelea kupeleka umeme katika maeneo ya vijijini yakiwemo maeneo ya miji yenye sura za vijiji.

Aidha, kwa maeneo ya Ugele, Mosi, Cargrielo, Machinjio, Ulonge, Mtalagala na Msisina yaliyopo katika Jimbo la Iringa Mjini, Serikali itayapelekea umeme kupitia mradi wa kupeleka umeme katika Vitongoji 15 kwa kila Jimbo.

SOMA: Kapinga aiagiza REA kufikisha umeme vitongojini

Ameongeza kuwa maeneo ya Cargrielo na machinjio yatapatiwa umeme na Tanesco kupitia miradi yake ya ndani ya kusogeza miundombinu ya umeme kwa wananchi.