Serikali kuja kivingine miundombinu viwanja vya ndege
KIGOMA: SERIKALI imesema itaendelea kujenga na kupanua miundombinu ya viwanja vya ndege ili kujihakikishia utoaji wa huduma ndani ya nchi na nchi jirani.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile wakati wa ziara yake ya kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo inayosimamiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Viwanja vya ndege nchini (TAA).
Katika ziara hiyo, Kihenzile amekagua upanuzi wa njia ya kuruka na kutua ndege kwenye uwanja wa ndege wa Kigoma, mkoani humo.
Amesema, serikali inachukulia sekta ya uchukuzi kwa njia ya anga kama mishipa ya ukuzaji uchumi na shughuli mbalimbali za utoaji huduma kwa wananchi ndani na nje ya nchi.
“Ndiyo maana imewekeza fedha nyingi kwenye maboresho,ukarabati na upanuzi wa viwanja vyetu vya ndege na ununuzi wa ndege kwa ujumla.
“Uchukuzi kwa njia ya anga ni uchumi pia diplomasia , kadri unavyojenga na kuboresha viwanja vya ndege ndivyo unavyojenga ushawishi kwa jamii inayokuzunguka ndani na nje ya nchi,” amesema Kihenzile
Aidha, Kihenzile amewataka wakala wa barabara nchini Tanroads na menejimenti ya uwanja wa ndege wa Kigoma kuhakikisha wanamsimamia mkandarasi kumaliza upanuzi huo kwa wakati na kiwango stahiki.
Awali Meneja wa uwanja wa ndege wa Kigoma, Mbura Daniel amesema kwa sasa uwanja huo unahudumia abiria 33,0000 kwa mwezi na miruko 102 hadi 105 kwa mwezi.
Amefafanua kuwa katika safari sita za juma, zinahusisha safari tatu za nje ya nchi hasa Burundi zikifanywa na shirika la ndege la taifa ATCL na kuongeza kuwa upanuzi wa uwanja huo utahusisha njia ya kuruka na kutua ndege kutoka mita 1800 hadi 3000.
Pia, eneo la megesho ya ndege , mnara wa kuongozea na jengo la abiria huku ukitarajiwa kuhudumia abiria 400,000 kwa mwaka na kuwekewa taa za kuongozea ndege ili utumike kwa saa 24.