Serikali kushirikiana na wadau agenda nishati safi

DAR ES SALAAM: SERIKALI imesema ipo tayari kushirikiana na kutoa msaada kwa wadau wa nishati wanaofanya juhudi za kusukuma mbele ajenda ya matumizi bora ya nishati nchini.

Hayo yalielezwa jana Dar es Salaam na Mkurugenzi Msaidizi, Sehemu ya Utawala katika Wizara ya Nishati, Wilson Nyamanga kwa niaba ya Katibu Mkuu wa wizara hiyo wakati wa uzinduzi wa awamu ya tatu ya programu ya ufadhili wa masomo kwa wanawake katika nishati endelevu.

Alisema programu hiyo inaisaidia serikali kusukuma mbele ajenda yake ya nishati safi na matumizi bora ya nishati.

 

“Programu hii inatujengea uwezo kwamba katika kusukuma ajenda ya nishati tuhakikishe kwamba wote tunashiriki kwa maana ya kuwa jumuishi, wanaume na wanawake wawepo kuhakikisha ajenda hiyo inatekelezwa,” alisema.

Alieleza kuwa Wizara hiyo ipo tayari kushirikiana na wanaotekeleza programu hiyo Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya na Ubalozi wa Ireland nchini kuhakikisha wanawake wengi wanaingia kwenye sekta ya nishati kwa ajili ya kusukuma mbele ajenda ya nishati.

Nyamongo aliongeza kuwa imezoeleka kuwa Tanzania, wengi waliopo katika sekta ya uhandisi ni wanaume lakini proramu hiyo imezalisha na inaendelea kuzalisha wahandisi wanawake watakaochangia kuimarisha sekta ya nishati nchini.

Akizungumzia programu hiyo, Mtaalamu wa Miradi wa UNDP, Tanzania Abbas Kitogo alisema ufadhili huo wa masomo ni kwa ajili ya wanafunzi wanawake watakaosoma Shahada ya Uzamivu katika masuala ya uhandisi wa nishati endelevu.

Alisema katika awamu ya kwanza walifadhiliwa wanafunzi 10 na awamu ya pili waliongezeka kufikia 25 na katika awamu ya tatu ambayo dirisha la maombi limefunguliwa rasmi jana hadi Septemba 15, watafadhiliwa wanafunzi wengine 10.

“Kama UNDP tunaliangalia hili kama jukumu kubwa kama shirika hasa katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa sababu nishati endelevu imesaidia sana kupunguza uzalishaji wa hewa chafu ambayo inasababisha mabadiliko ya tabianchi,” alisema.

Kwa upande wake Mkuu Msaidizi wa Ushirikiano katika Ubalozi wa Ireland, Helen Counihan alisema Ireland inajivunia kushirikiana na wadau wengine wa maendeleo katika kuwekeza kwenye kizazi kijacho cha kuendeleza nishati.

“Ireland inajaribu kuhakikisha inaweka mchango wake katika mabadiliko ya tabianchi na nishati endelevu na imedhamiria kuhakikisha malengo yaliyowekwa wakati programu hiyo inaanzishwa mwaka 2023 yanafikiwa. Kuwezesha wanawake katika sekta ya nishati si suala la usawa tu, bali ni uwekezaji katika ustahimilivu, ubunifu na mustakabali bora kwa wote,” alisema.

Nao wanufaika wa ufadhili huo ambao wanatarajia kumaliza masomo yao hivi karibuni Sherida Magomere na Zanura Miraji, walieleza kuwa ufadhili huo una manufaa si tu kwao bali ni uwekezaji kwa taifa kutokana na dhamira yao ya kuhakikisha sekta ya nishati inasonga mbele kupitia elimu waliyoipata.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button