Serikali kutathimini upya hekta 5,600 Bukombe

BUKOMBE: SERIKALI imepanga kufanya tathimini mpya ya eneo la hekta 5,693.7 ambalo lilimegwa kutoka hifadhi ya Biharamulo-Kahama na kuwapa wananchi kwa ajili ya shughuli za binadamu ili kukidhi mahitaji yao.
Hatua hiyo inakuja kufuatia kuibuka malalamiko mapya kutoka kwa wakazi wa kitongoji cha Idosero kijiji cha Nampalahala wilayani Bukombe wanaodai eneo walilopewa haliendani na mahitaji ya shughuli zao.
Mkuu wa mkoa wa Geita, Martine Shigella ametoa taarifa hiyo Agosti 30, 2025 mara baada ya kuwasili eneo la Beria lenye mvutano kati ya wananchi na Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) ili kutatua mgogoro huo.
Amesema uamuzi huo unalenga kufanikisha suluhu ya kudumu juu ya mgogoro huo ambao unapaswa kutatuliwa kwa mfumo shirikishi wa watalaamu na jamii badala ya kujikita kwenye mihemuko na kisiasa.
Shigella amesema serikali inatambua nafasi na umuhimu wa watanzania kupata maeneo rasmi ya makazi na uzalishaji ndio maana iliridhia kumega sehemu ya hifadhi na hivyo wananchi wanapaswa kuwa watulivu.
Asema iwapo tathimini itabaini eneo la Beria ambalo ni kilio cha wakazi wa Idosero ni sehemu ya hekta walizopewa basi utaratibu utafuatwa kuligawa lakini iwapo ni tofauti, basi maombi mapya yatahitajika.

“Kwa hiyo tuwe watulivu, hizo taratibu zifanyike kwa utulivu, kwa amani, kwa mshikamano, kwa ushirikishwaji, na zikikamilika mpewe taarifa, amesisitiza Shigella.
Ameagiza, wale ambao bado wana ukata wa maeneo ya kulima wanapaswa kuwasilisha maombi ofisi za TFS shamba la miti Silayo ili wapewe utaratibu wa kulima kwenye maeneo ya hifadhi kwa kufuata sheria.
Awali mkuu wa wilaya ya Bukombe, Pasikas Mulagiri alithibitisha kuwa mchakato wa kugawa hekta 5,693.7 zilizotolewa na serikali ulikuwa shirikishi na kila mwananchi alipatiwa eneo la makazi na kilimo.
Amesema eneo la makazi lilikuwa na viwanja 600 vilivyopimwa lakini wahitaji walikuwa takribani kaya 450 na wote walipatiwa na maeneo mengine yalitengwa kwa ajili ya shule, zahanati na huduma za jamii.
Ofisa Mhifadhi Mkuu wa Shamba la miti Silayo, Juma Mseti amesema TFS ilishatekeleza agizo la serikali la kumega hekta zilizotolewa na serikali kwa ajili ya shughuli za binadamu na sasa eneo lenye ulinzi ni hifadhi.
Mmoja ya wakazi wa Idosero, Self Mohamed amekiri kuwa mgogoro mkubwa uliopo haujatokana na wananchi kukosa makazi bali dhamira yao ni kurejea eneo la Beria ambalo walihamishwa na serikali.
Kwa upande wake Bundala Shabaan ameomba uongozi wa mkoa na wilaya kuliangalia jambo hilo kwa hekima na busara zaidi ili kuwezesha wananchi hao kuendelea na shughuli zao katika eneo la Beria.



