Serikali kutumia jitihada zote amani iendelee

RAIS Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuhakikisha mchakato wa mazungumzo ya maridhiano unafanikiwa ili kuwa na taifa lenye amani na umoja na kuendelea kuwa mfano wa utulivu katika Afrika na dunia kwa ujumla.

Hayo yalisemwa na Makamu wa Rais, Balozi Dk Emmanuel Nchimbi alipomwakilisha Rais Samia katika mkutano wa dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika kwa njia ya mtandao akiwa Dodoma.

Alisema serikali inayoongozwa na Rais Samia imechukua hatua za kurejesha utengamano katika nchi na kuhakikisha wananchi wanaishi katika utawala wa sheria.

“Tanzania ni salama na tulivu na ipo tayari kuendelea kupokea wageni kutoka duniani kote kwa manufaa ya nchi zote,” alisema.

Dk Nchimbi aliwashukuru viongozi wa SADC walioshiriki uapisho wa Rais Samia Novemba 3, mwaka huu na wote waliotoa pongezi za dhati, “Jitihada zote zitatumika kuhakikisha Tanzania inapata maendeleo na amani kuendelezwa,” alisema Dk Nchimbi.

Wajumbe wa mkutano huo pia walimpongeza Rais Samia kwa ushindi katika uchaguzi huo uliofanyika Oktoba 29.

Mkutano huo wa SADC ulilenga kujadili kujiondoa kwa Madagascar Unyekiti wa SADC. Afrika Kusini imependekezwa kuwa Mwenyekiti kwa kipindi cha mpito mpaka kufikia Agosti 2026.

Mkutano huo umekubaliana kuendelea kutumia kaulimbiu ya Mkutano wa 45 wa SADC uliofanyika nchini Madagascar ambayo ni ‘Kuimarisha viwanda, mapinduzi ya kilimo, mabadiliko ya nishati kwa SADC yenye uhimilivu’.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button