Serikali imeahidi kuupatia mchezo wa Judo vyumba vya kuchezea katika viwanja vya michezo nchini pamoja na kuratibu ufundishwaji wa Judo mashuleni kwa kushirikiana na wizara zinazosimamia shule.
Akizungumza leo jijini Dodoma, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Ndugu Said Yakub aliipongeza chama cha mchezo huo kwa utendaji bora ambapo ndani ya muda mfupi kimefanya mabadiliko makubwa ya kiutendaji.
“Chama cha Judo lazima kiwe taasisi kamili yenye mipango ya muda mrefu, muwe na mpango mkakati wa miaka mitano, muwe na kituo cha mafunzo, hapo litakuwa eneo ambalo mafunzo ya mchezo huo yatafanyika” alisema Naibu Katibu Mkuu.
Aidha, alimshukuru Rais wa Shirikisho la Judo Ulimwenguni Ndugu Marlus Vizer kwa kutoa msaada wake kwa mchezo huo huku akisema wamemualika nchini kwa lengo la kukutana na viongozi wa mchezo huo.
Kwa upande wake Rais wa Mchezo wa huo, Ndugu Hamisi aliahidi kutoa jozi 50 ya nguo za mchezo wa judo katika mashindano ya kimataifa, jozi 100 za nguo za mafunzo ya mchezo huo na jozi 200 za nguo za mazoezi kwa ajili ya wanafunzi.
Kwa kuongezea alisema kuwa Tanzania itapata nafasi ya kusomeshewa walimu wa mchezo huo kwa ngazi ya shahada. Judo ni mchezo wenye asili ya Japan huku ukichezwa sana katika mataifa ya Bara Ulaya ikiwamo Ufaransa