Serikali kuvuna bil 900/-mageuzi mashirika
MAGEUZI yanayoendelea kufanywa na serikali kwenye mashirika ya umma yameleta mafanikio na gawio kutoka kwenye taasisi hizo mwaka huu limefika zaidi ya Sh bilioni 900.
Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu alisema hayo Dar es Salaam wakati akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari kuhusu Siku ya Gawio itakayokuwa Juni 10, mwaka huu.
Rais Samia Suluhu Hassan atapokea gawio hilo Ikulu, Dar es Salaam kutoka mashirika ya umma zaidi ya 200 na lengo ni hadi ifikapo Juni 10, mwaka huu mashirika ya umma yatoe gawio la Sh trilioni moja.
“Ni dhahiri kuwa siku ya gawio imekuwa kichocheo kikubwa cha mageuzi na mafanikio tunayoyaona leo, tangu kuanzishwa kwa utaratibu huu wa wazi na wenye uwajibikaji, kumekuwa na ongezeko la mashirika yanayotoa gawio, pamoja na kuboreshwa kwa utendaji wao kwa ujumla,” alisema Mchechu.
Alisema hiyo ni ishara kuwa taasisi za umma zikisimamiwa kwa weledi, mafanikio ya kweli huonekana.
Mchechu alisema katika kipindi cha miezi 11 (Julai hadi Mei mwaka huu) mwezi mmoja kabla ya kumalizika kwa mwaka wa fedha 2024/2025, Ofisi ya Msajili wa Hazina imefanikiwa kukusanya Sh bilioni 884.7 mapato yasiyo ya kodi kutoka taasisi za umma na kampuni ambazo serikali ina umiliki wa hisa chache.
Alisema fedha hizo ni sawa na ongezeko la asilimia 40 ya makusanyo halisi kwa kipindi kama hicho kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ambapo ofisi hiyo ilikusanywa Sh bilioni 633.3. Mwaka jana,
Rais Samia alipokea gawio hilo la Sh bilioni 637 kutoka kwenye mashirika na taasisi 145 kati ya 304 zinazochangia asilimia 15 ya mapato ghafi na zile ambazo serikali ina hisa.
Kadhalika kwa miezi 11 mwaka huu kiasi kilichokusanywa na mapato yasiyo ya kikodi ni sawa na ongezeko la asilimia 15.3 ya makusanyo yote ya mwaka wa fedha 2023/2024 ambayo ni Sh bilioni 767.
Alitaja vyanzo vikuu vya mapato hayo kwa mwaka huu kuwa ni gawio la asilimia 63.9 ya mapato yote, michango ya asilimia 15 ya mapato ghafi ambayo ni asilimia 29.7 na mapato mengineyo.
Mapato hayo mengineyo yanajumuisha ziada, marejesho ya mikopo na riba pamoja na mawasilisho yatokanayo na mtambo wa kuhakiki na kuwezesha mawasiliano (TTMS) ni asilimia 6.4 ya mapato yote.
Akizungumzia sababu za ongezeko la mapato hayo kwa mwaka huu, Mchechu alisema limechangiwa na uimarishaji wa utaratibu wa ufuatiliaji wa karibu wa gawio na michango katika mashirika ya umma na matumizi ya mfumo wa Tehama.
“Ofisi imefanikiwa kuunganisha Mfumo wa Mpango na Bajeti (PlanRep) na Mifumo ya ERMS na e-Watumishi pamoja na kufanya maboresho ya Mfumo wa MUSE ambao unawezesha kupata taarifa halisi za matumizi katika taasisi na mashirika ya umma ili kuongeza uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa fedha za Umma,” alisema Mchechu.
Alisema mifumo hiyo inabadilishana taarifa ipasavyo na hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Rais Samia kuhakikisha mifumo inasomana.



