SERIKALI imesema itaendelea kushirikiana na madhehebu ya dini katika kuwaletea wananchi maendeleo.
Akizungumza leo wilayani Tandahimba mkoani Mtwara wakati wa kukabidhi fedha Sh milioni 100 zilizotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa msikiti wa Wilaya ya Tandahimba, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Patrick Sawala amesema nyumba hizo za ibada ni muhimu kwasababu wanawasaidia kuwalea kiimani.
“Nyumba hizi za ibada ni muhimu sana kwasababu ninyi mnatusaidia kutulea kiimani, kitukuza sisi kwa kuwa na maadili mema, kimwogopa Mwenyezi Mungu, kumtii na kufanya yale matendo ya mema yanayompendeza yeye”
Amesema hawana budi wote kushirikiana na kushikamana kama ambavyo wanatandahimba walivyoshirikiana katika ujenzi wa msikiti huo wa Rawdhwa unaojengwa wilayani humo.
Aidha ameendelea kuwaomba wadau mbalimbali kuendelea kuunga mkono jitihada hizo zilizofanywa na waumini hao ili uweze kukamilika ambapo kila mmoja kwa nafasi yake ni vizuri akachangia kwa kadri Mwenyezi Mungu atavyomjalia ili kukamilisha nyumba hiyo ya ibada.
“Katika kuthamini kazi yenu mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan naye amewaunga mkomo katika ujenzi wa msikiti huu, amethamini jitihada zenu kwa kuchangia Sh milioni 100″amesema Sawala.
Akitoa taarifa ya ujenzi huo, Mwenyekiti wa Kamati ya ujenzi huo, Kasim Lihumbo amesema ujenzi huo ni kupitia michango ya waumini na wadau mbalimbi ambapo hadi kukamilika utagharimu zaidi ya Sh milioni 400 ikiwa sasa upo katika hatua ya boma.
Kaimu Shekhe Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Jamaldin Chamwi amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuona jitihada hizo zinazofanywa wa waumini hao huku akisisitiza amani na utulivu kwa waumini na jamii kwa ujumla ili serikali iweze kuwapatia msaada kwa kile wanachokifanya.
“Kwa hili sisi waislamu tunatakiwa tujifundishe jambo, mahala popote palipo na utulivu watu wakashikamana, wakaungana serikali inaona kinachofanywa tunaweza tukasaidiwa katika njia mbalimbali”amesema Chamwi.